Dar es Salaam. Bao la Straika wa Taifa Stars, Wazir Junior mapema tu dakika ya tano, limetosha kuizamisha Zambia nyumbani kwao katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 uliochezwa leo Jumanne Juni 11, 2024.
Mchezo huo wa Kundi E uliochezwa Uwanja wa Levy Mwanawasa uliopo Zambia, Taifa Stars ilitumia vyema shambulizi lao la kwanza dakika ya tano ambapo Mudathir Yahya alimpokonya mpira Kings Kangwa na kwa haraka akampasia Wazir ambaye aliuweka nyavuni.
Kuingia kwa bao hilo, kuliamsha zaidi hasira kwa Zambia ambao waliingia uwanjani kwa ajili ya kuhakikisha ushindi lazima waondoke nao kutokana na kufahamu kwamba kupoteza kwao itawaweka katika hali mbaya zaidi kwenye msimamo kwani wametoka kufungwa 2-1 na Morocco.
Mashambulizi kadhaa ya nyota wao, Patson Daka ambaye alipiga mipira ya vichwa minne kipindi cha kwanza, hayakuzaa matunda kwani timu zilienda mapumziko matokeo yakiwa Zambia 0-1 Stars.
Kipindi cha pili, Taifa Stars ilifanya mabadiliko ya mapema dakika ya 46 akitoka Mudathir Yahya ambaye alimaliza kipindi cha kwanza akiwa amepata maumivu, nafasi yake ikachukuliwa na Adolf Mtasingwa.
Hadi kufika dakika ya 59, Taifa Stars ilifanya mabadiliko ya wachezaji wanne ambapo mbali na Mudathir kutoka, wengine waliofuatia ni Himid Mao, Wazir Junior na Simon Msuva ambao nafasi zao zilichukuliwa na Abdul Sopu, Charles M'mombwa na Edwin Balua.
Zambia waliendeleza mashambulizi yao kipindi cha pili lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Taifa Stars ikiongozwa na Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto, lango lilikuwa salama chini ya kipa Ally Salim ambaye alifanya sevu kadhaa za hatari ikiwemo ile ya dakika ya 89 kutoka kwa Kings Kangwa.
Ushindi huo kwa Taifa Stars umewafanya kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi E kutoka ya nne baada ya kufikisha pointi sita sawa na vinara Morocco, tofauti ni mabao ya kufunga na kufungwa. Timu zingine zilizopo katika kundi hilo ni Niger, Zambia na Congo, huku Eritrea ikiondolewa.
Huo ulikuwa ni mchezo wa tatu kwa Taifa Stars katika harakati za kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, michuano itakayofanyika nchi za Marekani, Canada na Mexico, wakati Zambia kwao ulikuwa wa nne. Taifa Stars imeshinda mechi mbili na kupoteza moja wakati Zambia ikipoteza tatu na kushinda moja pekee jambo linalomuweka kwenye wakati mgumu Kocha Avram Grant.
Timu tano za Kundi E zinawania nafasi moja ya juu ili kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2026. Ikumbukwe kuwa, katika makundi tisa yaliyopangwa, vinara watafuzu moja kwa moja, wakati washindi wanne bora 'best loser' watakaobaki watacheza kwa mfumo wa mtoano na mshindi atashiriki Mashindano ya FIFA Play-off kuwania nafasi ya kufuzu.