Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Watu wenye umri wa miaka 40 au zaidi na hawana hela hawapaswi kumlaumu Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwakuwa watu hao wamezaliwa wakati Mwl. Nyerere akiwa madarakani na vimepita vipindi vingi hivyo hawapaswi kumlaumu Rais ambaye ana miaka mitatu tu kwenye Uongozi wake.
Akiongea mbele ya Rais Samia leo June 11,2024 wakati wa upokeaji wa gawio na michango kutoka Mashirika na Taasisi za Umma Ikulu Jijini Dar es salaam, Chalamila amesema;
“Mh. Rais nikushukuru kwa Uongozi wako, tumekufuatilia katika ziara kadhaa ukiwa Ufaransa na ukiwa Korea hii juzi, umefanya ziara yenye tija kubwa kwa Taifa letu, maneno yanaweza kuwa ni mengi lakini hivi juzijuzi wachache walionisikiliza nilisema ukiona una miaka 40 au zaidi na hauna hela usimlaumu Mh. Rais wa Tanzania (Dkt. Samia Suluhu Hassan)”
“Nilimaanisha umezaliwa wakati wa Mwl Nyerere vimepita vipindi vingi vya kiuongozi na kama haukuwa na hela kwanini umlaumu Mtu ambaye ana miaka mitatu tu katika Uongozi wake?, na kikubwa nilichokitaka ni kwamba wajibu wa Serikali ni kuandaa mazingira rafiki ili kukusaidia wewe kuchemka na fursa zilizoletwa na Serikali na kwamba lawama ni tamko la laana linalokufanya ujisahau pale ulipokosea na kutojisahihisha ukidhani upo hivyo ulivyo kutokana na sababu ambazo sio za kweli”
“Mh. Rais sisi Wananchi wa Dar es salaam tunakuthibitisha kwamba Mkoa huu utaendelea kuwa salama, salama kisiasa, kiuchumi, kijamii na salama kwa Watu wanaoishi katika Mkoa huu na tunafanya hivi kwasababu Mkoa huu ni potential”