WAKATI mchakato wa usajili wa wachezaji wa ndani na nje ya Tanzania kuelekea maandalizi ya msimu mpya ukiendelea, unaweza kusema Wekundu wa Msimbazi wanawachelewesha watani zao, Yanga kumtangaza kiungo, Clatous Chama, ametua katika timu yao, imeelezwa.
Chama amekataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Simba kwa sababu hawajafikia kiwango cha fedha ambacho amekihitaji wakidai hastahili kulipwa kutokana na umri na kiwango chake cha sasa huku tetesi zikieleza Mzambia huyo tayari ameshamalizana na Yanga.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema wanachelewa kutangaza majina ya wachezaji walioachwa na wapya ambao wamewasajili kutokana na baadhi ya klabu kutokamilisha mchakato wa kuachana na nyota wao.
Kamwe bila kutaja majina, alisema kuna klabu zinachelewa kuwapa barua za 'kwaheri' nyota wao kwa hofu ya kujiunga na Yanga na hali hiyo imezua wasiwasi kwa wanachama na mashabiki wa Simba hasa wapi anakwenda kiungo huyo.
"Kuna mchezaji mmoja anamaliza mkataba, lakini jamaa hawataki kumpa barua, wana hofu atakuja kwetu, wampe tu kijana wa watu ili aje kwenye klabu ya ndoto yake, na hilo ndilo limetufanya mpaka sasa tuahirishe au tuchelewe kuwapa 'Thank You' tutakaoachana nao na kutangaza wachezaji wapya ambao tumewasajili," alisema Kamwe.
Taarifa kutoka Simba zinasema mkataba wa Chama na Simba umebakiza siku chache na sasa kanuni zinamruhusu kufanya mazungumzo na timu yoyote inayohitaji huduma yake.
"Mkataba wa Klabu ya Simba na Chama unamalizika ifikapo Juni 30, na baada ya hapo anakuwa huru, ameshazungumza na Yanga, pande zote mbili zimekubaliana wanasubiri mkataba wake uishe ndiyo atie wino, ameshakubaliana nao ada ya usajili na mshahara na posho nyingine muhimu, kinachosubiriwa ni muda tu," kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliendelea kusema huenda 'upepo' ukabadilika na Chama ambaye hii si mara ya kwanza anahusishwa kutua Jangwani, anaweza kubakia Msimbazi na 'kuzika' ndoto za Yanga kupata huduma ya mchezaji huyo.
"Awali hawakufikia mwafaka na Chama, lakini mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka upande wa mwekezaji ambaye pia yumo katika Kamati ya Usajili ameliingilia kati suala hilo.
Siku mbili zilizopita, mazungumzo kati ya Chama na uongozi yalianza tena, yamekwenda vizuri, maslahi ya mchezaji yamezingatiwa, ninachokwambia mpaka sasa bado hajasaini mkataba, ila ameridhia kubaki, kinachosubiriwa ni saini, dole gumba na kuanza kupiga picha ya utambulisho," kiliongeza chanzo hicho.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema hakuna mchezaji anayetakiwa kubaki na klabu hiyo ataondoka.
Ahmed alisema Kamati ya Usajili inajipanga kuimarisha kila idara katika kikosi chao kwa ajili ya kuongeza nguvu na kufikia malengo kwenye msimu mpya wa mashindano.
"Ukiona mchezaji yoyote wa Simba ameondoka ujue hatumhitaji, kama yupo kwenye malengo yetu hawezi kuondoka," alisema ofisa huyo.
Aliongeza wako katika hatua za mwisho za kukamilisha wachezaji wanaowahitaji pamoja na kutangaza kocha mkpya ambaye ataongoza benchi la ufundi la timu hiyo.
Tayari Simba imeshatangaza itaenda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya katika mji wa Ismailia, ulioko Misri ukiwa na kikosi kamili.