UVCCM Waomba Serikali Kufunga Mtandao wa Twitter Nchini




JUMUIYA ya Umoja Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wameiomba Serikali kufungia mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter usifanye kazi Tanzania kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanakwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.

Hayo amesemwa leo June 11,2024 na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Kawaida alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema wanatishwa na mienendo ya mtandao huo kutokana na kuweka maudhui ambayo hawaridhishwi nayo.

Amesema kwanza kabisa inaonyesha wazungu walituandaa kisaikolojia kuuona mtandao huo ni wa kawaida baada ya kuubadilisha jina kutoka twitter na kuuita X.

"Hivyo kutokana sisi ÚVCCM kubeba dhamana ya vijana nchini tunaona mtandao huu unakuja kuharibu vijana ambao ni nguvu kazi ya kesho" amesema

Hivyo amesema Jumuiya hiyo wanaiomba serikali kusitisha matangazo ya mtandao huo nchini Tanzania.

"Hatuko tayari kupoteza desturi zetu kama vijana tuko tayari kulinda desturi na mila zetu na kulinda nguvu kazi ya Taifa hasa vijana" amesema Kawaida

Kijana Khalfani Mussa (29) mkazi wa jijini Dar es Salaam ameiambia Nipashe kuwa endapo serikali itafungia mtandao huo ambao UVCCM wameingiwa shaka nao itakuwa vyema kwani mitandao hiyo imekuja kuharibu vijana nchini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad