Zuberi Msemo, akiwa na watoto wake waliopoteza maisha.
WATUMISHI wawili wa Kituo cha Afya Levolosi, jijini Arusha, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za kushindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha watoto watatu wa familia moja kupoteza maisha katika ajali ya moto iliyotokea Juni 22, mwaka huu.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea taarifa kutoka katika mitandao ya kijamii Juni 23, mwaka huu, mwananchi akilalamika kucheleweshwa kupatiwa huduma kwa wagonjwa watatu wa ajali hiyo waliofikishwa katika kituo hicho siku ya tukio.
Taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini, ilieleza kuwa watumishi hao wanapisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kushindwa kutekeleza majukumu yao.
"Waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni Fatma Amir (mtumishi aliyekuwa eneo la mapokezi) na Kamwana David (Ofisa Tabibu aliyetoa huduma ya matibabu)," alisema mkurugenzi huyo katika taarifa hiyo.
Hamsini alisema timu ya kufuatilia tuhuma hizo tayari imeshaundwa na ripoti itawasilishwa kwa mwajiri.
Mkurugenzi huyo pia ametoa maelekezo kwa watumishi wote wa umma kuzingatia weledi na maadili ya utumishi wa umma wanapotoa huduma kwa wananchi.
Juni 22, mwaka huu, watu wanne wa familia moja, wakazi wa Mtaa wa Olmatejoo, jijini Arusha, walipoteza maisha akiwamo askari wa daraja la kwanza wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) anayefanya kazi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, baada ya makazi yao kuteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, chanzo cha moto huo ni kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa katika soketi ya umeme, kushika moto na kuunguza kochi.
Mbali na kusababisha vifo pia, moto huo pia ulijeruhi watu wengine saba, akiwamo mtoto mchanga wa siku nne, ambao walikimbizwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru).
Waliopoteza maisha ni baba mzazi wa watoto hao, Zuberi Msemo, aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini huko na watoto wake; Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3).
Majeruhi wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Mount Meru ni mama wa watoto hao, Jasmine Khatibu (33), Mariam Mussa (60), ambaye ni mama mzazi wa Zuberi na Mwanaid Aldina (50), Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na mfanyakazi wa ndani aliyefahamika kwa jina moja la Easther (20).