Wakenya kutoka maeneo ya Kisumu, Kisii, Mombasa na sehemu nyingine za nchi wamejitokeza tena barabarani ili kuonyesha kutoridhika kwao na serikali ya Rais wa nchi hiyo Wiliam Ruto. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kauli mbiu ya #occupystatehouse imekuwa ikipamba moto kwenye mtandao wa kijamii wa X huku hali ya taharuki ikiendelea kuibuka jijini Nairobi.
Hayo yanajiri siku moja baada ya Rais Ruto kutangaza kurejesha bungeni muswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao ndio chanzo cha maandamano hayo yaliyoibua hasira za vijana wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Barabara zinazoelekea katika ikulu ya rais zimefungwa ili kuwazuia waandamanaji wanaokadiria kuzuru ikulu ya rais leo Alhamisi.
Maafisa wa vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) wameonekana katika maeneo tofauti ya jiji kuu la Nairobi huku wakiwa na zana za vita licha ya mjadala mkali ulioibuka kuhusu kuwekwa kwa maafisa wa KDF katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Hata hivyo, hali ya utulivu umeshuhudiwa katika maeneo mengine ya nchi ikiwemo Nairobi ambapo maandamano makali yalishuhudiwa juzi Jumanne.
“Siku ya leo imekaa vibaya tuko kwenye maandamano kwa sababu vijana wenzettu waliuawa bila sababu hata sasa hatujapewa majibu ya maswali yetu ndio maana bado tunalia,” amesema mama mchuuzi wa mboga Linet Moraa alipozungumza na Citizen.
Muswada wa kuidhinisha kutumika kwa majeshi ya KDF ambao umepitishwa na bunge la nchi hiyo limeibua mjadala mkali huku mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo akikosoa uamuzi huo akisema kuwa ni kinyume na katiba ya Kenya.
Vilevile, alisema kuwa wabunge walioidhinisha muswada huo haikufika 50 kama katiba ya nchi hiyo inavyoagiza ikiwamo kurusha mubashara ‘live’ matangazo ya bunge hilo kama ilivyofanyika kwa miswada mingine.
“Ruto aache kuwadanganya wakenya. Tumesoma bwana! Katika katiba ya Kenya rais ana majukumu mawili ya kukataa ama kukubali hakuna kitu kama kutoa muswada,” alisema mwandamanaji mmoja katika kaunti ya Mombasa akiiambia NTV.