Wanne Wafariki Ajali Gari aina ya Toyota Noah




WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Noah iliyokuwa imebeba ng'ombe aliyechinjwa kwa ajili ya sikukuu ya Eid Al Adha kugonga lori kwa nyuma

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema ajali hiyo imetokea Juni 19, 2024 saa 3:00 usiku katika kijiji cha Kwae kata ya Msisi Halmashauri ya Wilaya ya Singida barabara kuu ya Singida- Mwanza.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya gari Toyota Noah lenye namba za usajili T 674 CSY iliyokuwa na abiria wanane na ngo'mbe aliyechinjwa kuligonga kwa nyuma lori la mizigo aina ya Mercedes Benz lenye namba T 352 DDP mali ya kiwanda cha kusindika pamba kilichopo Manispaa ya Singida.

Kamanda Kakwale alisema baada ya Toyota Noah kuligonga lori hilo gari jingine aina ya Toyota Carina lenye namba za usajiri T 143 TLV iliyokuwa ikiendeshwa na Elias Zabron ambaye ni Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara nalo ililigonga Noah hiyo kwa nyuma.

Aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Kidanka Ntandu ambaye alikuwa dereva wa Toyota Noah, Ally Ibrahimu (40) mkazi wa Singida mjini,James Muro (45) mkazi wa Makiungu na mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka 50 ambaye jina lake halijafahamika.

Alisema miili ya watu hao waliofariki imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, majeruhi wa ajali hiyo ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali hiyo ni Omari Jumanne mkazi wa Singida, Ramadhani Kisuda (36) mkazi wa Singida, Joseph Kim (45) mkazi wa Makiungu na Athuman Salehe (41) mkazi wa Majengo Singida.

Kamanda Kakwale alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Noah ambaye alikuwa mwendo kasi alishindwa kulimudu na hivyo kuligonga lori kwa nyuma.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad