Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema anaridhishwa na utendaji kazi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na kuwataka wengine kuiga mfano na kuwa wabunifu katika kutatua kero za wananchi.
Ametoa kauli hiyo jijini wakati wa uzinduzi wa Programu ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa gharama ya Sh. bilioni 400.
Mchengerwa amesema, "Nipende kuweka wazi -ninafurahishwa na utendaji wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha (Makonda), hilo bila kuficha nimesema ukweli, ninaomba (mwakilishi) fikisha salamu hizo."
Mchengerwa amewataka wakuu wa mikoa na watendaji wengine wa mamlaka za serikali za mitaa nchini kuhakikisha wanaongeza kasi ya usikilizaji kero za wananchi na kuzitatua.
"Nchi hii ni ya wananchi, hakuna namna, niliwaambia ukiwa mkuu wa mkoa au kiongozi ndani ya serikali, ukijishusha cheo chako hakiwezi kuondoka, kitabaki palepale, lakini tutaendelea kuongeza imani kwa wananchi na kulinda na kuongeza kura.
"Tunatambua yapo maeneo wasaidizi wetu hawajatuelewa vizuri, hatuna budi kuwasaidia ili waweze kutuelewa maana kuna wengine wanahisi masuala mengine si yao, mfano miradi, hivyo hii lazima tukairekebishe," amesema.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa kila mkuu wa mkoa ana hulka ya utendaji kazi. Hata hivyo, serikali inataka kuona kero zikitatuliwa moja kwa moja kwa wananchi kule chini na kuwe na utendaji wa ubunifu ili kupunguza malalamiko kwa wananchi.
Kuhusu programu hiyo, waziri huyo amesema inalenga kuamsha chachu ya utendaji kazi katika maeneo yao ya utawala.
"Rais ametuletea programu hii ili tuboreshe maeneo ya utendaji kazi wetu, kazi tuliyobaki nayo ni utoaji huduma na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja," amesema.
Waziri huyo amesema uanishwaji wake ni mwendelezo wa juhudi za serikali kupanua wigo wa ugatuaji madaraka kwa wananchi kwa kuimarisha Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.