Yanga Kulipiza Kisasi, Kuwaleta Mamelodi Sundowns Siku ya Wananchi

Yanga Kulipiza Kisasi, Kuwaleta Mamelodi Sundowns Siku ya Wananchi


KLABU ya Yanga imetajwa kukamilisha usajili wa golikipa wa Ihefu FC, ambayo kwa sasa imebadili jina na kuitwa Singida Black Stars, Khomein Abubakar, kuchukua nafasi ya Metacha Mnata huku pia ikitangaza kuileta Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Wiki ya Mwananchi Agosti, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kuwa kama mambo yatakwenda yalivyopangwa basi safari hii Yanga itakipiga dhidi ya timu hiyo ambayo ilicheza nayo katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika michezo miwili Dar es Salaam na Afrika Kusini, timu zote zikishindwa kufungana kabla ya wawakilishi hao wa Tanzania kuondolewa kwa mikwaju ya penalti 3-2.

"Kama alivyosema siku chache nyuma Rais wa Klabu, Injinia Hersi kuwa tuna mwaliko Kenya kwa ajili ya kwenda kufungua uwanja na Afrika Kusini ambako tumealikwa na Mamelodi Sundowns, sasa na sisi pia tumeamua kuwaalika kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi kuelekea msimu ujao wa mashindano, kama mambo yataenda kama yalivyopangwa tutakipiga nao siku hiyo," alisema Kamwe.

Wakati hayo yakiendelea, chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kinasema klabu hiyo imemsajili, Khomein baada ya mapendekezo ya benchi la ufundi chini ya Miguel Gamondi, akiwa ni mchezaji wa kwanza Mtanzania kusajiliwa na Yanga msimu huu.

"Ilikuwa ni lazima kwanza tupate kipa mzawa ili awe mbadala wa Diarra, na kulikuwa na machaguo kadhaa ambayo tumeyakosa, hatimaye tumeangukia kwa Khomein, ila ni mmoja wa makipa wazuri sana, alionyesha kiwango kikubwa msimu huu akiwa na kikosi cha Ihefu, mpaka benchi la ufundi likatoa pendekezo la kusajiliwa," kilisema chanzo hicho.

Taarifa zinasema awali, Yanga ilikuwa ikimhitaji kwa udi na uvumba golikipa wa Prisons, Yona Amosi, ikashindikana, baadaye ikahamia kwa kipa wa Geita Gold, Costantine Malimi na mwishoni ikaangukiwa kwa Khomein.

Kabla ya kujiunga na Ihefu, Khomein alikuwa kipa wa Geita Gold ambako alifanya vema akiwa langoni.

Yanga pia inatajwa kuwa mbioni kumsajili winga wa timu hiyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Emmanuel Bola Lobota, aliyekuwa kwenye kiwango cha juu msimu huu, hasa baada ya kumkosa Philippe Kinzumbi wa TP Mazembe ambaye ameikacha timu hiyo na kutimkia, Raja Casablanca ya Morocco.

Wengine wanaotajwa kuwa huenda wanaweza kuvaa uzi wa kijani na njano ni kiungo mshambuliaji, Charve Onoya na kiungo mkabaji, Agee Basiala, wote wanakipiga katika Klabu ya AS Maniema Union na beki wa kushoto, Chadrack Boka kutoka Klabu ya Saint Eloi Lupopo, wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad