Baleke, Chama Wauwasha Moto Licha ya Kufungiwa



Dar es Salaam. Licha ya Yanga kufungwa katika mechi ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki ya Kombe la Mpumalanga, lakini kikosi hicho kimeonyesha shoo ya maana Sauzi, huku kocha Miguel Gamondi ameanza mapema kumuamini kiungo mshambuliaji kutoka Simba, Clatous Chama, huku Jean Baleke akitumia dakika 22 tu uwanjani kufungua akaunti ya mabao akiwa na uzi wa timu hiyo.

Yanga ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-1 na FC Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, katika pambano la kwanza la michuano ya Kombe la Mpumalanga lililopigwa kwenye Uwanja wa Mbombela, Mpumalanga huko Afrika Kusini, huku kocha Gamondi akimuanzisha Chama pekee miongoni mwa nyota wapya na kuwaanzishia benchini Jean Baleke, Prince Dube, Duke Abuya, Chadrack Boka, kipa Abubakar Khomeiny na Aziz Andambwile kabla baadhi yao kuwaingiza kipindi cha pili.

Licha ya kutoonyesha makeke yaliyozoeleka kutokana na soka la wapinzani wao wanaoshiriki Bundesliga, lakini Chama alionekana wakati fulani kuwasumbua mabeki wa timu pinzani ikiwamo kutoa pasi murua ya dakika ya 36 kwa Maxi Nzengeli ambaye alipiga shuti kali lililogonga nguzo na kurudi uwanjani kisha Stephane Aziz Ki kurejesha kombora kali lililotolewa na kipa Daniel Klein.

Yanga katika mchezo huo, ilicheza soka la kushambulia kwa kushtukiza na ilikatika eneo la katikati pengine ni kutokana na kukosekana kwa Khalid Aucho ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akisaidiana na Mudathir Yahya, huku Wajerumani wakicheza soka la pasi ndefu na kushambulia muda mwingi, japo mabeki wa vijana wa Jangwani walituliza na kuokoa hatari zote za Augsburg.

Hata hivyo, licha ya Yanga kuokoa hatari nyingi za wapinzani wao, ilijikuta ikifungwa bao la kwanza katika dakika ya 38 kupitia kwa beki Mads Pedersen aliyepiga shuti la chini kutokea pembeni kushoto lililompita kipa Diarra Djigui.

DAKIKA 64 ZA CHAMA

Kocha Gamondi alimuanzisha Chama na ndani ya muda huo, hakuonyesha kiwango kibovu wala kikubwa sana, akifanya yake kwa kutoa pasi za uhakika ambapo pasi yake moja ya mwisho nusura iipe Yanga bao katika dakika ya 36 ya kipindi cha kwanza akimpa Maxi lakini shuti la Mkongomani huyo likagonga mlingoti wa lango.


Mastaa wa Yanga, Augsburg wakiwa katika picha ya pamoja baada mchezo wa kirafiki kumalizika katika Uwanja Mbombela, uliopo Mpumangala Afrika Kusini. Picha na Yanga
BOKA, ABUYA NOMA

Beki wa kushoto Chadrack Boka naye alicheza mchezo huo akiingia kipindi cha pili kilipoanza akichukua nafasi ya mwenzake Nickson Kibabage.

Beki huyo alionyesha ubora wake wa kupandisha mashambulizi mbele pamoja na kurudi kwa haraka kukaba kwa haraka.

Mbali na Boka kiungo mzawa Aziz Andambwile naye alipewa muda kama huo akichukua nafasi ya Mudathir Yahya ambapo alionyesha kiwango kizuri akiziba vyema eneo la katikati kutopitika kirahisi na Wajerumani hao.

Kiungo mpya Mkenya Duke Abuya naye alipewa muda kama huo akionyesha ubora mkubwa wa kukimbiza mpira kwenda eneo la wapinzani sambamba na kutoa pasi zilizofika vizuri, huku shuti lake kali la dakika ya 54 lilikuwa ni shambulizi zuri kwa timu yake.

BALEKE NA BAO

Bao pekee la Yanga lilifungwa katika dakika ya 64 na mshambuliaji mpya Jean Baleke aliyeingia kipindi cha pili kumpokea Chama na kucheza mechi ya kwanza akiwa na uzi wa Yanga na akadhihirisha Wananchi hawakukosea kumsajili kwani alitumia dakika 22 tu uwanjani kufunga bao pekee la kufutia machozi.

Baleke alifunga bao hilo kwa kichwa kikali katika dakika ya 86 akiunganisha vyema krosi ya kiungo Nzengeli, japo dakika mbili nyuma alikosa umakini kumalizia pande jingine na Dube.

DUBE BAO LA WAZI

Mshambuliaji mpya wa Yanga, Prince Dube aliyeingia kipindi cha pili alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango.

DIARRA NA MAXI

Kipa wa Yanga, Diarra aliyecheza mchezo mzima, alikuwa shujaa muhimu kwa timu yake akiokoa mashambulizi mengi ya hatari akidhihirisha kwamba timu yake haijakosea kumuongezea mkataba mwingine wa mwaka mmoja.

Mbali na Diarra, pia viungo Maxi, Stephanie Aziz KI walionyesha kwamba bado wako kwenye kiwango bora huku mabeki Yao Kouassi na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ nao walikuwa imara kwenye ukuta.

MASHUTI MATANO

Hadi mapumziko Yanga ilikuwa imepiga shuti moja pekee lililolenga lango lakini mpaka mchezo huo unamalizika ikawa imepiga mashuti matano yaliyolenga lango.

Yanga itacheza mchezo wa pili Julai 24 itakapocheza mechi ya pili ya kirafiki ya mashindano hayo dhidi ya wenyeji wao TS Galaxy.

BAO LA AUGSBURG

Dakika ya 80 ilimtoa tena Clement Mzize ambaye alisumbua ngome ya Augsburg licha ya kukosa umakini kukwamisha mpira wavuni, kumpisha Shekhan Ibrahim, japo haikusaidia kuizuia Augsburg kuandika bao la pili dakika ya 81 kupitia Tietz aliyemalizia pasi murua ya Okugawa.

Yanga haikukata tamaa na badala yake iliendelea kusumbua na dakika ya 86 ndipo ilipata bao la kufutia machozi.

Vikosi vilivyoanza:

AUGSBURG: Klein/Jager, Pedersen/Petkov, Gouweleeuw/Bauer, Rexhbecaj/Pfeiffer, Mounie/Banks, Breithaupt/Dorsch, Jensen/Maier, Engels/Komur, Essende/Okugawa, Schlotterbeck/Kabadayi na Koudssou/Tietz

YANGA: Diarra, Yao, Kibabage/Boka, Bacca, Job/Mwamnyeto, Sure Boy/Andambwile, Maxi, Mudathir/Abuya, Mzize/Shekhan, Chama/Baleke na Aziz KI/Dube

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad