Dar es Salaam. Bei ya petroli imeshuka mwezi huu Julai katika mikoa inayochukua mafuta hayo Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na Juni, huku dizeli ikiongezeka kidogo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha kuwa bei za mafuta kuanzia leo Jumatano Julai 3, 2024 yale yanayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam petroli imeshuka kwa Sh51 kwa lita na kuwa Sh3,210 huku dizeli ikiongezeka kidogo kwa Sh3, kutoka Sh3,112 hadi Sh3,115 katika mkoa huo.
Kwa ile inayochukua petroli katika bandari ya Tanga, bidhaa hiyo imeshuka kutoka Sh3,263 Juni hadi Sh3,210 Julai na kwa ile inayotegemea Bandari ya Mtwara nayo imepata ahueni kutoka Sh3,267 hadi Sh3,212 katika kipindi sawa na hicho.
Hata hivyo, dizeli inayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka kutoka Sh3,121 Juni hadi Sh3,124 Julai, pia kwa yale yanayopitia Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,122 hadi Sh3,124 katika kipindi kama hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule kupitia taarifa kwa umma aliyoisaini amesema miongoni mwa sababu za kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo ni kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 5.92.