Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akiongea na Chama. Picha ya kuunganisha ni ya Dube.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ametahadharisha kuwa kuelekea msimu ujao atapanga kikosi chake kutokana na kiwango cha mchezaji na jinsi anavyojituma kwenye mazoezi na si jina la mtu.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwa na maswali kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo wakifikiria nani ataanza kwenye kikosi cha kwanza kutokana na aina ya usajili uliofanywa kukiimarisha kikosi hicho.
Yanga imewaongeza kikosini, kiungo Clatous Chama aliyeachana na Simba baada ya mkataba wake kumalizika na mshambuliaji Prince Dube ambaye aliamua kuvunja mkataba wake na klabu ya Azam FC.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya kwanza ya kikosi hicho juzi kwenye ufukwe wa bahari maeneo ya Coco, Miguel, alisema kama kuna mchezaji anatarajia kucheza kwa sababu ya jina lake asahau, badala yake atapanga kikosi kutokana na kile kilichoonyeshwa kwenye uwanja wa mazoezi, pamoja na kiwango anachokionyesha uwanjani.
Gamondi alisema, amefurahi kuona kikosi chake kimeongezewa wachezaji mahiri kiasi cha kutompa tabu kupanga kikosi.
"Kila kocha anaona furaha kuwa na wachezaji bora, angalia kuna Chama, Pacome (Zouzoua), Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Mudathir (Yahaya), Khalid Aucho, ila kuwapanga inategemea na mpinzani unayoenda kucheza naye na kiwango chake, kwangu mimi hakuna kucheza kwa sababu ya jina bali kiwango, nataka kila mchezaji aonyeshe kiwango chake ili kuwa katika kikosi cha kwanza," alisema Kocha huyo.
Hata hivyo, amewataka mashabiki pamoja na wapenzi wa timu hiyo kuwa na subira na wachezaji wapya kwani pamoja na uwezo wao, wanahitaji muda ili waweze kuonyesha kile walichokuwa wakikifanya katika timu walizotoka.
"Tunatakiwa kuwa wavumilivu kwa sababu wanatakiwa kujua mbinu zetu za kimchezo na kufahamiana na wenzao, nafikiri watu wasiwe na haraka kuwaona wachezaji wapya wakicheza vile wanavyotaka wao, kwani katika soka baadhi ya wachezaji hawana muda wa kusubiri, ukiwaweka tu uwanjani wanacheza vizuri, lakini wengine wanahitaji muda," alisema Gamondi.
Kuhusu mfumo wa uchezaji, alisema yeye kama mwalimu ndiye anayejua atawatumia vipi na si mtu mwingine yoyote, na katika timu lazima kuwe na uwiano.
"Kuna muda unahitaji ucheze na mastraika watatu au viungo watatu wa kushambulia au wawili, inategemea wachezaji na jinsi ulivyowafundisha na kocha unavyotaka.
Watu wanawaza kutaka fulani na fulani wacheze, hapana siwezi kufanya hivyo, unajua kocha anatakiwa kuifanya timu kuwa na uwiano, msimu uliopita tulicheza mechi 50, hivyo tuna michezo mingi sana msimu ujao, hivyo kuna muda atacheza Aziz Ki, wakati mwingine Chama, au Dube, kuna muda hawatacheza kwa sababu huu ni mpira, ninachofurahi kama kocha ni kuwa na machaguo mengi, nina uhakika kiwango chetu kitaongezeka hasa kwenye michezo ya kimataifa," alisema Gamondi.