Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive Jijini Dar es Salaam imeutaka upande wa Jamhuri katika kesi ya ukahaba inayowakabili Watu watano kutekeleza amri zake ikiwemo kuwasilisha taarifa ya kitabibu ya Shahidi wao wa nne.
Hakimu Mfawidhi, Lugano Kasebele amesema hayo leo July 08,2034 wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusiana na amri hizo za Mahakama, ambapo amesema endapo ikifika July 11, 2024 Jamhuri ikishindwa kutekeleza basi anaweza kuifuta kesi hiyo.
Miongoni mwa amri hizo ni upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa Shahidi wake wa nne katika kesi hiyo, WP Konstebo (PC) Masadi Kassim wa kituo cha Polisi Magomeni Usalama.
Pia kuwafikisha Mahakamani uthibitisho wa Mashahidi wake wengine ambao pia ni Maaskari Polisi waliodawa kuwa wako kwenye
kazi maalumu, katika kesi hiyo, Washtakiwa ni Mariam Mkinde (25) Mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) Mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) Mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) Mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) Mkazi wa Ubungo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.