Klabu ya Simba huenda ikaendelea kubaki na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho raia wa Cameroon, Leandre Essomba Onana kwa msimu ujao.
Awali, ilielezwa Onana aliyejiunga na Simba akitokea Rayon Sports, huenda angeondoka baada ya kushindwa kufanya vizuri, lakini sasa mabosi wa Simba watakutana naye kujadiliana mustakabali wao kwa msimu ujao.
KLABU ya JS Kabylie ya Algeria, ipo katika mazungumzo ya kupata saini ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Babacar Sarr.
Msenegal huyo kwa sasa ni mchezaji huru na endapo dili lake hilo la kutua JS Kabylie litakamilika, ataungana na aliyekuwa kocha mkuu wa Simba Mualgeria, Abdelhak Benchikha na kiungo Sadio Kanoute.
KLABU ya Pamba iko katika hatua nzuri ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Mofosse Tresor Karidioula.
Nyota huyo mwenye uraia wa Ivory Coast na Burkina Faso, tayari amewasiliana na mabosi wa Pamba huku ikielezwa wamekubaliana kimaslahi na kilichobaki ni kusaini mkataba na timu hiyo.
FOUNTAIN Gate imeanza mazungumzo ya kumbakisha beki wa kati wa timu hiyo, Abdulmajid Mangalo baada ya mkataba wake kuisha.
Mangalo aliyewahi kung'ara na Biashara United, inaelezwa ameigomea ofa aliyowekewa baada ya kupata ofa nyingine za Tabora United ya Tanzania, Gor Mahia na Kakamega Homeboyz za Kenya.
TIMU ya Kagera Sugar, iko mbioni kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Joseph Mahundi.
Nyota huyo wa zamani wa Azam FC, Mbeya City na Coastal Union kwa sasa ni mchezaji huru, huku ikielezwa tayari Kagera wameshazungumza naye ili atue kwa wakata miwa hao.
KAGERA Sugar, iko hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa beki wa kati wa Tanzania Prisons, Chilo Mkama.
Beki huyo aliyewahi kuzichezea timu kadhaa kwa mafanikio zikiwemo za Toto Africans, Mbao, Polisi Tanzania na Geita Gold, kwa sasa ni mchezaji huru hivyo kuzivutia klabu mbalimbali zinazomuhitaji japo Kagera ndio iko mstari wa mbele kumnasa.
WINGA machachari wa zamani wa Simba, Kagera Sugar aliyekuwa Geita Gold iliyoshuka daraja, Yusuph Mhilu, inadaiwa ameahirisha mipango ya kurejea kwa wakata miwa na sasa kusalia Geita kucheza Ligi ya Championship.
Inadaiwa Mhilu yupo katika mazungumzo ya kusalia hapo na huenda akapewa mkataba wa mwaka mmoja na kufuta mipango ya kuondoka katika klabu hiyo iliyoshuka daraja sambamba na Mtibwa Sugar.