Joto la Uchaguzi Lapanda TLS, Wengine Wapinga Kuondolewa Mwabukusi





JOTO la uchaguzi wa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), limeendelea kupanda, huku baadhi ya mawakili wakipinga kuenguliwa kwa mgombea wa nafasi hiyo, Boniface Mwabukusi.


Tofauti na vyama vingine vya kitaaluma, uchaguzi wa TLS umekuwa na mguso wa pekee kwa jamii ukitikisa ndani ya chama na kwenye mitandao ya kijamii.

Jana, wakili Peter Kibatala, alisema kuenguliwa kwa Mwabukusi kunaufanya uchaguzi uwe na maswali mengi kwa kuwa tuhuma za maadili zilizomwengua, hazina mashiko.

Alisema kuishtaki serikali ni jambo la kawaida wala hakupingani na sheria wala Katiba ya nchi.

Akizungumza na Nipashe jana, Kibatala alisema kamati iliyomwengua ina uwezo wa kumrejesha kuwania kiti hicho, akikumbusha kuenguliwa kwa aliyekuwa mgombea urais wa TLS, John Seka, mwaka 2016.

“Sio lazima awe mgombea wangu na wala nisingemchagua Mwabukusi kwa sababu zangu…kama unakumbuka kamati iliwahi kumwengua John Seka, nikasimama ukumbini kuiambia kamati kwamba walikosea kumwondoa, wakamrejesha na akashinda urais, maana yake ni kwamba walimwengua mtu ambaye alikuwa chaguo la watu na wasingemrejesha ni kwamba tungepata mtu asiye sahihi,” alisema.

Alisema mawakili wanatumia njia za kisheria kudai haki. “Sisi sio marubani au madaktari, tutajua nini cha kufanya maana ndicho tulichokisomea.”

Awali, katika andiko lake kwenye mitandao ya kijamii, Kibatala alisema ataendelea kupinga mchakato wa uchaguzi na kususia mikutano akieleza kuwa chama hicho ndio ukuta wa mwisho wa kuulinda umma.

“Nitashiriki kuwashawishi wengine wafanye hivyo, kwa wakati huu nitashirikiana na wakili Mwabukusi katika kusaka haki yake ya kisheria. Kwa hali ilivyo, sioni kuna uchaguzi halali ndani ya TLS,” alisema Kibatala.

Mmoja wa wagombea urais, Kapteni Ibrahim Bendera, alisema uamuzi wa Mwabukusi kwenda mahakamani ni sahihi kwa kuwa ni chombo cha kutoa haki.

“Hatuwezi kulazimisha kamati imrejeshe, lakini naamini mahakamani atapata haki stahiki. Mwenyewe keshasema atakata rufaa, tusubiri maamuzi ya mahakama na matokeo ya rufaa,” alisema.

Alisema anawania ili aongoze Baraza la Uongozi kuboresha taaluma ya uwakili; kuwasaidia na kuwaelimisha mawakili wenye uzoefu wa chini ya miaka mitano ambao hawaruhusiwi kuingia Mahakama ya Rufani; kupunguza ada ya kila mwaka; kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuwekeza kwenye vitega uchumi katika kila tawi la TLS.

Kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wanaharakati wameunga mkono uamuzi wa Mwabukusi kushinikiza arejeshwe kuwania nafasi hiyo, wakieleza kuwa ana haki kisheria na kikanuni.

SARAKASI

Kwa miaka mingi, uchaguzi wa TLS umekuwa ukivuta hisia za wananchi ndani na nje ya chama hicho, huku sarakasi zikitawala.

Mwaka 2016, Seka alienguliwa na baada ya mawakili ‘kuijia juu’ kamati ya uchaguzi, ilimrejesha na akachaguliwa kuongoza chama hicho.

Uchaguzi wa TLS umekuwa wa mchakamchaka kutokana na majukumu yake ambayo ni pamoja na kuishauri serikali na taasisi zake. TLS ilianzishwa kwa sheria mwaka 1954 kama chama cha kitaaluma cha mawakili nchini na kifungu cha 4 cha sheria hiyo (Sheria ya Chama cha Mawakili wa Tanganyika), inabainisha majukumu makuu matatu ya taasisi hiyo.

Jukumu la kwanza, ni kuwaunganisha, kuwatetea na kusaidia ustawi wa mawakili nchini. Pili, ni kuishauri Serikali na vyombo vyake kama Bunge na Mahakama. Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Kutokana na nguvu hiyo, chama hicho kimekuwa kikipitia nyakati tofauti za viongozi kulingana na wakati husika. Kuanzia mwaka 2016, TLS ilikuwa na viongozi waliokuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali akiwamo Fatma Karume, ambaye jina lake lilienguliwa mwaka 2019.

Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania. Majukumu hayo yanasababisha jamii ifuatilie kwa ukaribu uchaguzi wake.

Baadhi ya viongozi wa TLS waliokuwa mwiba kwa serikali ni pamoja na Tundu Lissu, aliyekuwa Rais wake mwaka 2017, na katika kipindi chake, kulikuwa na msuguano mkali kati ya TLS na serikali.

Serikali iliituhumu TLS kufanya siasa kwa kukosoa kazi zake, badala ya kujielekeza kwenye malengo ya kuanzishwa kwake, jambo ambalo lilizidisha migongano baina ya pande hizo mbili.

Kutokana na hali hiyo, Machi 2017, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alitishia kukifuta chama hicho.

Hata hivyo, baada ya Lissu, mwanaharakati ambaye alikuwa mkosoaji wa serikali, Fatma Karume, alichaguliwa kuiongoza TLS.

Mwaka uliofuata, alisimama kutetea nafasi yake kwa awamu nyingine, lakini jina lake halikurejeshwa.

Wakati wa uongozi wa Fatma, misuguano kati ya TLS na serikali ilishika kiasi cha kuonekana chama hicho kimebeba agenda za kiharakati.

Septemba 20, 2019, Fatma alisimamishwa uwakili na Mahakama Kuu kwa madai ya kuishambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na alifikishwa mbele kamati ya maadili ya mawakili kujadiliwa. Kamati hiyo ilimfutia uwakili, hata hivyo, alirejeshewa tena Juni 21, 2021.

Baada ya Karume, alichaguliwa Profesa Edward Hosea, aliyekuja na sera ya sera ya majadiliano ya kujenga, kwa maana ya kukaa pamoja na serikali ambayo ni mdau muhimu ili kufanyakazi kwa ushirikiano, na katika uchaguzi wa kwanza, Hosea aliibuka kidedea kwa kumwangusha aliyeonekana kuwa mpinzani wake mkubwa, Harold Sungusia.

Sungusia ndiye rais wa TLS anayemaliza muda wake wa uongozi akiwa amehudumu vipindi viwili mfululizo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad