Kaizer Chifes Wamemtamani MAX Nzengeli Huenda Wakamaliza na Yanga Huko Huko Afrika Kusini

 

Kaizer Chifes Wamemtamani MAX Nzengeli Huenda Wakamaliza na Yanga Huko Huko Afrika Kusini

Kiwango bora kinachoonyeshwa na nyota wa Yanga, Maxi Nzengeli, raia wa DR Congo, kimewavutia mabosi wa Kaizer Chifes walioamua kupiga hodi na kuulizia uwezekano wa kumsajili winga huyo katika dirisha hili la usajili.


Maxi ambaye ni miongoni mwa wachezaji muhimu zaidi ndani ya Yanga kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi uwanjani, anatakiwa na Kaizer Chiefs ambayo hivi karibuni ilimtambulisha Nasreddine Nabi kuwa kocha wao mpya.


Taarifa ilizozipata Mwanaspoti kutoka Afrika Kusini ambapo Yanga imepiga kambi tangu Julai 18, mwaka huu, zinabainisha kwamba kati ya wachezaji wa timu hiyo walioonekana kuwa vizuri, Kaizer imeanza na Maxi.


Mmoja wa watu ndani ya Yanga amebainisha kwamba ishu ya kumsajili Maxi ni pendekezo la Nabi ambaye amekuwa akimfuatilia kabla hata nyota huyo hajatua Yanga msimu uliopita akitokea Maniema ya DR Congo.


“Yanga ina wachezaji wengi wazuri, lakini viongozi wa Kaizer wameona kwanza waanze na Maxi kwa sababu amependekezwa na Kocha Nabi anayetaka kumuweka kikosini kwake ili kukiimarisha zaidi,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza:


“Nabi anamfahamu Maxi tangu akiwa DR Congo akicheza Maniema kabla ya kutua Yanga, lakini hawajawahi kufanya kazi pamoja kwa sababu wakati Nabi anaondoka mwisho wa msimu uliopita, Maxi ndiyo akasajiliwa Yanga.”


Ikumbukwe kwamba, Nabi ambaye alitambulishwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga Aprili 20, 2021, alidumu kikosini hapo hadi Juni 15, 2023 kabla ya kutimkia FAR Rabat ya Morocco aliyoinoa kwa msimu mmoja na hivi sasa kuibukia Kaizer Chiefs.


Ndani ya Yanga, Nabi alibeba makombe mawili ya Ligi Kuu Bara na mawili ya Kombe la Shirikisho (FA), huku akiifikisha timu hiyo kwa mara ya kwanza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.


WALICHOKIONA KAIZER


Tangu ajiunge na Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2023-2024, Maxi amekuwa mchezaji muhimu kikosini jambo ambalo timu nyingi ikiwemo Kaizer Chiefs zimeonekana kuvutiwa naye.


Maxi ambaye kiasili ni winga akicheza kushoto na kulia, pia ana uwezo wa kutumika katika kulinda mashambulizi langoni kwao akicheza kama beki wa kushoto katika mfumo wa 3-5-2 ambapo hupanda na kushuka.


Uwezo wake wa kukaba, kupandisha mashambulizi na kushuka kuzuia ni silaha kubwa kwake huku akibebwa zaidi na kazi aliyonayo.


Pia ni mzuri katika kufunga kwani katika msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga amefunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu Bara.


VIGOGO KUMALIZANA


Kwa mujibu taarifa ni kwamba, kwa kuwa Yanga bado ipo Afrika Kusini ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya (pre-season), mabosi wa timu zote mbili wanatarajia kukutana kumalizana juu ya ishu hiyo.


“Mazungumzo juu ya dili hilo bado hayajafanyika, lakini yanatarajiwa kufanyika wikiendi hii baada ya mchezo wao wa kirafiki kumalizika,” alisema mtu huyo aliyepo Afrika Kusini.


Jumapili, wiki hii, Yanga itacheza mechi ya tatu ya kirafiki ikiwa Afrika Kusini dhidi ya Kaizer Chiefs katika kuwania Kombe la Toyota.


Kabla ya mchezo huo, Jumamosi iliyopita ilicheza na FC Augsburg ya Ujerumani na kupoteza kwa mabao 2-1, huku kesho Jumatano ikiwa na kibarua cha kuikabili TS Galaxy. Mechi hizo mbili ni za Mpumalanga Cup.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad