Dar es Salaam. Edgar Mwakabela maarufu Sativa anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kisha kumtesa, kwa mara ya kwanza tangu apatikane Juni 27 ameandika katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter).
Sativa aliyepatikana Katavi akiwa na majeraha baada ya kutoweka jijini Dar es Salaam leo Julai 7, 2024 ameandika;
"Asante bwana kwa uzima huu hakika nimeliona jina lako. Sifa na utukufu ni kwako bwana.
"Kaponye wagonjwa mahospitalini, kalinde watumiaji wa barabara na vyombo vya usafiri wakawe salama," ameandika Sativa.
Sativa ameongeza; "Katuletee wateja kwenye biashara zetu, kalinde watoto wetu watokapo majumbani na warudipo."
Kijana huyo mkazi wa Mbezi anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha, alifanyiwa upasuaji Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kupata mpasuko wa taya la kushoto.
Akizungumza na Mwananchi jana Julai 6,2024 mratibu wa matibabu ya Sativa, Martin Masese maarufu ‘MMM’, amesema Sativa ameruhusiwa kurudi nyumbani na atatakiwa kurejea kliniki baada ya siku saba na kisha baada ya siku 14 ataondolewa nyaya alizowekewa kwenye taya.
“Atarudi kliniki baada ya siku saba, baada ya siku 14 pia atarudi akaondolewe nyaya kwenye taya lake,” amesema Martin.
Kwa upande wake, Wakili wa Sativa, Paul Kisabo kupitia mtandao wake wa X alikoweka picha akiwa na Sativa ameandika: “Tunawashukuru madaktari waliomtibu,@Sativa25, tuendelee kumuombea.
Kwa sasa ataendelea na kliniki Aga Khan Hospital. Tunahitaji tume huru iundwe ili kuchunguza na kuhakikisha wahusika wote waliomteka, kumtesa na kumpiga risasi wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” ameandika Wakili Kisabo kupitia mtandao wake wa X.
Kupitia chapisho lake Sativa, watu mbalimbali wamempa pole na kuonesha kufurahishwa na kurudi kwake tena katika mtandao wa X.
@TanzaniaOneJezi ameandika “Mungu ni mwema pole sana mzee Mwenyezi Mungu hamtupi mja wake hakika Mungu alisimama na wewe alikuwekea ulinzi katika pori lenye wanyama wakali.”
Naye @awesially ameandika, “Kaka pole sana, Mungu kaonyesha miujiza juu yako😪 karibu tena kaka ndugu zako tunakupenda sana👏.”