Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limedai aliyehusika na shambulio la risasi kwa mgombea urais wa Chama cha Republican, Donald Trump ni kijana mwenye umri wa miaka 20.
FBI ambayo imesema uchunguzi bado unaendelea, umemtaja kijana huyo kwa jina la Thomas Matthew Crooks.
“Alitoka Bethel Park huko Pennsylvania eneo ambalo jaribio la mauaji lilitokea. Bado uchunguzi unaendelea,"imesema taarifa ya awali FBI.
Hata hivyo, taarifa ya FBI imesema mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na maofisa wa FBI.
Tukio la Trump kushambuliwa lilitokea jana Jumamosi jioni Julai 13, 2024 akihutubia huko Butler.
Trump ambaye ni Rais wa zamani wa Taifa hilo, alikuwa akihutubia kwenye mkutano ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake kabla ya uchaguzi mkuu wa taifa hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la VOA, Trump alionekana akinyoosha mkono wa kulia kuelekea shingoni kabla ya tukio hilo.
"Damu imeonekana usoni na kwenye sikio la kulia. Maofisa wa ulinzi walifika jukwaani na kumzingira kwa haraka," imeeleza VOA.
Umati wa watu ulimshangilia wakati akiondolewa jukwaani na kupelekwa kwenye gari lake, huku akiinua mkono wake kuonyesha ishara ya ushindi.
Hayo yamejiri ikiwa ni siku moja kabla ya kongamano kuu la Chama cha Republican lililopangwa kufanyika kuanzia Jumatatu mjini Milwauke, Wisconsin, ambapo Trump anatarajiwa kutangazwa rasmi kama mgombea urais kuelekea uchaguzi wa Novemba mwaka huu.