Wakili Boniface Mwabukusi (katikati) akisherekea na mawakili wezake baada ya kushinda rufaa yake wakiwa katika chumba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Dar es Salaam. Wakili Boniface Mwabukusi sasa ni ruksa kugombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Hatua hiyo inatokana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutengua uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TLS, iliyomwengua kugombea nafasi hiyo Julai 5, 2024.
Kwa uamuzi wa mahakama, sasa Mwabukusi atachuana na wagombea wengine watano waliopitishwa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 2, jijini Dodoma.
Mawakili hao ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba.
Shauri hilo mahakamani ni kama limemsaidia Mwabukusi kufanya kampeni, kwani tangu alipoanza mchakato wa kimahakama Julai 11, 2024 amekuwa akiungwa mkono na mawakili wenzake kadhaa wakihudhuria mahakamani, mbali na wengine 29 waliomwakilisha mbele ya jaji.
Awali, aliwasilisha maombi ya kufungua shauri la marejeo ya uamuzi uliomwengua kwenye orodha ya wagombea urais wa TLS, ndipo aliruhusiwa na kufungua shauri ambalo limehitimishwa leo Julai 26, 2024.
Hata baada ya mahakama kubatilisha uamuzi uliomwengua kuwa mgombea, baadhi ya mawakili wameeleza utayari wao kwenda kumpigia kura.
Mwabukusi alienguliwa katika kinyang'anyiro hicho na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TLS kutokana na rufaa aliyoikata Wakili Bosco Mahai, akipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TLS iliyompitisha Mwabukusi, ikitupilia mbali pingamizi dhidi yake.
Kamati ya Rufaa mbali na kutupilia mbali rufaa ya wakili Mahai na kukubaliana na hoja za mawakili wa Mwabukusi, kuwa mrufani hakuwa na haki ya kisheria kuweka, Kamati hiyo iliibua hoja mpya kuwa Mwabukusi hana sifa kwa kuwa alishatiwa hatiani kwa suala la maadili na Kamati ya Mawakili, hivyo ikamwengua.
Suala hilo, ndilo Mwabukusi aliwasilisha Mahakama Kuu kama shauri la marejeo ya uamuzi uliomwengua, kusaka haki yake ya kugombea wadhifa huo.
Hukumu ya suala hilo imetolewa leo Ijumaa, Julai 26, 2024 ikitengua uamuzi wa kumwengua.
Mwabukusi aliyewakilishwa na jopo la mawakili 29, alitoa hoja mbili kupinga uamuzi wa Kamati ya Rufaa, akieleza haikuwa na mamlaka ya kumuondoa kugombea baada ya kupitishwa, na kwamba aliondolewa bila kupewa haki ya kusikilizwa.
Mahakama katika uamuzi uliotolewa na Jaji Butamo Phillip, imekubaliana na hoja za Mwabukusi kuwa kamati haikuwa na mamlaka ya kumwengua.
Jaji Phillip amesema hakuna sheria inayoipa mamlaka Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TLS kumwondoa mgombea katika uchaguzi, bali mamlaka yake ni kutupilia mbali rufaa inayopelekwa mbele yake, kama haina mashiko.
Amesema iwapo ina mashiko, inapaswa kurejesha mapendekezo kwa Kamati ya Uchaguzi.
Amesema kama kungekuwa na sheria inayotoa mamlaka hayo ingeitaja.
Jaji amesema mahakama pia inakubaliana na hoja za mawakili kuwa kamati hiyo ilifanya uamuzi bila kumpa Mwabukusi fursa ya kusikilizwa, hivyo uamuzi kama huo hauwezi kusimama.
"Nimekubaliana na mawakili wa mwombaji kuwa haki ya kusikilizwa ilipuuzwa, kitu ambacho kwa msimamo wa kisheria huwezi kukichezea. Kwa hiyo haki ya kusikilizwa ilikiukwa… maamuzi kama hayo hayawezi kusimama," amesema Jaji Phillip.
Amesisitiza kuwa uamuzi wowote unaofanywa bila kutoa haki ya kusikilizwa wa upande mmoja, unakuwa umekiuka kanuni ya haki asili ambayo ni ya muhimu.
Amesema uamuzi kama huo ni batili na hauwezi kuachwa ukasimama hata kama ungekuwa sahihi au hata kama mwombaji angesikilizwa uamuzi ungekuwa huohuo.
"Kwa hiyo uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa TLS wa Julai 5, 2024 unabatilishwa na kutupiliwa mbali," amesema.
Akizungumzia uamuzi huo, mmoja wa mawakili wa Mwabukusi, Jebra Kambole amesema kwa uamuzi huo, sasa unaosimama ni wa Kamati ya Uchaguzi wa TLS ambayo ilishampitisha kuwa mgombea wa urais.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TLS, Francis Stolla amesema wakili Mahai aliyemwekea pingamizi Mwabukusi hana hatua yoyote anayoweza kuichukua baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
"Kama ambavyo Kamati ya Rufaa iliamua, yeye hakuwa na haki ya kisheria kuweka pingamizi. Kwa mujibu wa kanuni, mwenye haki ya kuweka pingamizi ni mgombea mwenzake, wakala wa mgombea au mtu aliyempendekeza mmoja wa wagombea," amesema Stolla ambaye pia ni rais mstaafu wa TLS.
Hoja hiyo imeungwa mkono na wakili Edson Kilatu ambaye pia alimwakilisha Mwabukusi kwenye shauri hilo akisema msimamo huo umewekwa na Kanuni ya 50 ya Tangazo la Serikali namba 598 la mwaka 2022.
"Sasa Mahai hakuwa mgombea, hakuwa wakala wa mgombea yeyote wala hakuwa amempendekeza mgombea yeyote, kwa hiyo hakuwa na sifa ya kumwekea pingamizi mgombea yeyote," amesema Kilatu.
Kwa upande wake, mmoja wa mawakili walioiwakilisha TLS katika shauri hilo, Steven Mwakibolwa ameieleza Mwananchi kuwa wanakubaliana na uamuzi wa mahakama.
"Uamuzi wa Mahakama sisi tumeupokea na tunaukubali, maana ni uamuzi wa haki. Mahakama imetenda haki," amesema Mwakibolwa.
Kauli ya Mwabukusi
Mwabukusi amesema uamuzi wa kuondolewa katika kinyang'anyiro ulikuwa hauungwi mkono na TLS, bali ulifanywa na watu wachache.
Ametoa wito kwa mawakili wote kwenda Dodoma siku ya uchaguzi kumpigia kura awe rais, akiahidi kuifanya TLS iwajibike kwao na kwa jamii.
Amesema atapigania masilahi na haki za mawakili wote bila ubaguzi.
Shangwe mahakamani
Uamuzi huo umepokewa kwa shangwe na mawakili waliojitokeza mahakamani wengine wakiweka wazi kuwa wako tayari kwenda kumpigia kura Mwabukusi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Vijana (AYL), Edward Heche amesema wana imani na Mwabukusi, kwamba kulingana na misimamo yake ataibadikisha TLS na kuifanya itimize wajibu wake wa kuishauri Serikali, Bunge na Mahakama, mambo ambayo yalikuwa hayatekelezwi.
"Kwa hiyo mimi kama mwenyekiti wa mawakili vijana ninatoa wito mawakili vijana wote twende Dodoma tukampigie kura Mwabukusi,” amesema.
Happiness Michael, kwa upande pia ametoa wito kwa mawakili kwenda Dodoma kumpigia kura Mwabukusi awe rais wao.
Wakili Abdon Rwegasira amesema hakuwa na mpango wa kwenda kwenye uchaguzi huo, lakini baada ya uamuzi wa mahakama sasa atakwenda Dodoma kumpigia kura Mwabukusi.
Mmoja wa wagombea wa nafasi ya AYL, Emmanuel Ukashu amelieleza Mwananchi kuwa baada ya uamuzi huo ameshapokea simu za mawakili 15 wanaouliza mipango ya usafiri wa kwenda Dodoma kwenye uchaguzi.