Klabu ya Simba SC imethibitisha kuwa golikipa Ayoub Lakred raia wa Morocco atazidi kusalia kunako Klabu ya Simba msimu ujao.
Akithibitiosha hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa Ayoub Lakred ambaye mkataba wake ulikuwa umemalizika, ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Simba.
“Lakred ameongezewa mkataba atakuwa kwenye sehemu ya kikosi lakini yeye atajiunga na wachezaji wengine akitokea Morocco kwa kuwa tumeona kutakuwa na ugumu mkubwa kwenye suala la usafiri mpaka arejee hapa kuanza safari na wachezaji wengine," amesema Ahmed.
Ipo wazi kwamba awali Lakred ilikuwa inatajwa kuwa kipa huyo yupo kwenye hesabu za kurejea Morocco ambapo kuna timu kubwa zilikuwa zinawania saini yake.
Miongoni mwa timu ambazo zilitajwa kuweka dau kubwa la mkwanja kumnasa kipa huyo ni pamoja na Raja Casablanca jambo lililokuwa likiongeza presha kwa mashabiki wa Simba kukosa huduma ya mchezaji huyo.
Lakred kwenye mechi za mwanzo hakuanza kwenye ubora wake jambo lililopelekea Kariakoo Dabi mzunguko wa kwanza asikae langoni badala yake kipa namba moja Aishi Manula alianza.
Kwenye mchezo huo baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-5 Yanga kikiwa ni kipigo kikubwa kwa Simba kwa msimu wa 2023/24. Kwenye mzunguko wa pili alikaa langoni na ubao ukasoma Yanga 2-1 Simba.
Timu ya Simba chini ya Kocha Mkuu Fadlu Davids imekwea pipa kueleka Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2024/25 na mwamba huyo atajiunga moja kwa moja na wachezaji wenzake akitokea Morocco kwa mujibu wa Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano.