Kocha Mkuu wa Augsburg Awasifu Yanga..Wachezaji Wanauwezo Binafsi



WAKATI Kocha Mkuu wa Augsburg, Jess Thorup, inayocheza Ligi Kuu ya Ujerumani Bundlesliga, akiimwagia sifa Yanga kutokana na kiwango ilichoonyesha katika mechi ya juzi nchini Afrika Kusini, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema bado anaendelea kutengeneza kikosi kwani ana muda mfupi tu tangu aanze maandalizi, lakini akiridhishwa na vijana wake.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi maalum ya kuwania Kombe la Mpumalanga, ukichezwa Uwanja wa Mbombela, nchini humo na Yanga kupoteza kwa mabao 2-1, Gamondi alisema pamoja na kikosi chake kuwa na siku chache tu tangu kianze maandalizi, lakini ameridhishwa na kiwango hasa kipindi cha pili.

"Kwetu tumeupokea vizuri huu mchezo kwa sababu usisahau tumecheza na timu ya kiwango cha juu sana, hii timu huwa inacheza dhidi ya Bayern Munich, Leverkusen na Dortmund, kwetu sisi ndio kwanza tunaanza maandalizi na nimeona tumekuwa tunapoteza mipira kirahisi, lakini ni kawaida kwa hatua hii ya maandalizi," alisema Gamondi.

Alisema ameridhishwa na viwango vya wachezaji wake kwani katika muda huu ambao wanarejea kutoka majumbani wakati mwingine baadhi wanakuwa hawapo vizuri.

"Kwa ujumla nimeridhishwa na viwango vya wachezaji wangu, kipindi cha kwanza wapinzani wetu walipoteza nafasi kama tatu hivi, sisi tulipoteza mbili, kipindi cha pili tulitawala na kutengeneza nafasi ambazo tungeweza kusawazisha hata dakika za mwisho," alisema raia huyo wa Argentina.

Naye kocha wa Augsburg ambayo msimu uliomalizika ilikamata nafasi ya 11 katika Ligi Kuu ya Ujerumani, Thorup, aliimwagia pongeza Yanga, akisema ina wachezaji wenye nguvu, wanaocheza soka la kasi, lakini baadhi wakiwa na vipaji binafsi.

"Yanga ni timu nzuri, ina wachezaji wenye nguvu, baadhi wana vipaji binafsi, wana kasi na wanacheza kwa kasi sana na hata bao lao la kufutia machozi lilikuwa bora sana.

"Nashukuru tulimiliki mpira dakika 45 za kwanza, kipindi cha pili kwangu hakikuwa kizuri hatukuweza kumiliki kama cha kwanza, Yanga wakimiliki mchezo kipindi hicho," alisema kocha huyo.


Mabao ya washindi yalifungwa na beki wa kushoto raia wa Dermark, Mads Pedersen, dakika ya 37, na winga wa kushoto Mjapan Masaya Okugawa, akapachika bao la pili dakika ya 80, huku straika Mkongomani Jean Baleke, akifunga bao la kufutia machozi dakika nne kabla ya mechi kumalizika baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Mkongomani mwenzie, Maxi Nzengeli.

Yanga itaingia tena dimbani Jumatano kucheza dhidi ya TS Galaxy na Jumapili Julai 28, itamaliza mechi zake nchi humo kwa kucheza dhidi ya Kaizer Chiefs, mechi ya Kombe la Toyota, kwenye Uwanja wa Bloemfontein.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad