Kocha Mokwena wa Wydad Aukubali Mziki wa Fei Toto



Kocha Mkuu wa Wydad Casablanca ya Morocco, Rhulani Mokwena, ameonekana kuvutiwa zaidi na uchezaji wa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', huku akisema amegundua kitu kingine kwake, ambacho ni utu na upole tofauti na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa kama wake.


Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya timu hizo mbili uliochezwa juzi, Benslimane nchini Morocco ambako Azam imeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, kocha huyo mpya wa Wydad, alisema amekuwa akimfuatilia mchezaji huyo mara kwa mara, na amemvutia, na siku hiyo amemwona mwenyewe mubashara uwanjani.


"Kwangu katika bara hili, Feisal ni mchezaji wa kipekee sana si tu kama mwanasoka, pia napenda utu wake, kiubinadamu ni mtu mzuri sana, mpole ni wachezaji mastaa wachache sana Afrika unaoweza kuwakuta wana tabia kama yake, wengi ni watata sana," alisema Mokwena ambaye msimu uliopita alikuwa akiifundisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.


Katika mechi ya juzi, Azam ilikubali kipigo cha mabao 4-1, mchezo ambao hadi mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.


Akizungumzia mchezo huo, alisema ulikuwa mzuri na mgumu, ambapo Azam wamempa mechi nzuri ambayo imemfanya kuona mazuri na mapungufu ya kikosi chake.


"Naishukuru Klabu ya Azam, imenipa mechi nzuri, ilikuwa mechi kali na yenye kasi kubwa, nimeona uwezo wao na wachezaji wao, wanapambana sana, kwa hili walilolionesha hata wao wanaweza kufanya vema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema.


Tayari Azam imeshacheza mechi tatu za kirafiki ikiwa kwenye kambi ya maandalizi nchini humo, awali ilikipiga dhidi ya US Yacoub Al Mansour ya Ligi Daraja la Tatu nchini Morocco, ikishinda mabao 3-0, kabla ya kucheza na timu ya Ligi Kuu, Union Touarga Sport na kutoka sare ya bao 1-1.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad