Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya madai ya mwanamuziki Lameck Ditto dhidi ya kampuni ya Multchoice Tanzania Limited maarufu DStv.
Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Julai 16, 2024 ikaaihirishwa. Hukumu hiyo sasa itatolewa leo Julai 22, 2024 mahakamani hapo mbele ya Jaji Mfawidhi, Salma Maghimbi.
Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bwakeya, alifungua kesi ya madai mwaka 2020 akiiomba Mahakama iamuru kampuni Multichoice Tanzania (DStv) imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo wa 'Nchi Yangu' aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara, bila ridhaa yake wakati wa kampeni za fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.
Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.
Katika kesi hiyo, Ditto alipeleka mashahidi watano na DStv ilikuwa na mashahidi wawili--- Astrid Mapunda na Johnson Mshana wakiongozwa na mawakili, Simon Lyimo na Thomas Mathias.
Upande wa Ditto, baadhi ya mashahidi wake walikuwa ni mtayarishaji wa wimbo huo, Emmanuel Maungu (Emma the boy), meneja wake, Rodney Rugambo na Angela Karashani wakiongozwa na mawikili, Ally Hamza na Elizabeth Mlemeta.
Mlemeta ameiambia Mwananchi Digital kuwa hukumu hiyo itatolewa leo saa 4 asubuhi, ikiwa ni baada ya kuwasilisha hoja za mwisho kuhusiana na ushahidi na utetezi uliotolewa.
"Juni 24, tuli-file closing submissions (mawasilisho ya hoja za mwisho) na kilichobaki tunasubiri hukumu leo saa 4 asubuhi," amesema.