Manabii Wacharuka, Wawajibu Wanaowasema Mitandaoni

 

Manabii Wacharuka, Wawajibu Wanaowasema Mitandaoni

Baadhi ya manabii na mitume wamefunguka wakati wa ibada wakijibu watu wanaozungumzia huduma wanazozitoa.


Wiki hii kumekuwa na maoni tofauti kwenye mitandao ya kijamii kuhusu huduma zinazotolewa na viongozi hao wa dini zikihusishwa na kujipatia ukwasi mkubwa.


Mwananchi pia imeandika mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu huduma hizo, zikihusisha utozaji wa fedha ili kuwaona viongozi hao na hata kuwauzia waumini maji, mafuta, chumvi na vitambaa.


Nabii Kiboko ya Wachawi


Nabii Dominic ‘Kiboko ya Wachawi’ amesema amekuwa akisumbuliwa na waandishi wa habari wakimtaka ajibu madai yanayoelezwa na baadhi ya viongozi wa dini kuhusu huduma yake lakini hakuwahi kuwajibu.


"Mungu ana maajabu yake kati ya mtu anayesemwa na anayesema, mara nyingi Mungu anamuongezea anayesemwa ndicho kinachotokea hapa kwangu kila siku watu wanaongezeka," amesema


Amesema hakuna Kanisa au Msikiti wenye haki miliki ya waumini, isipokuwa kila mtu ana uhuru wa kwenda kuabudu popote ilimradi asivunje katiba na sheria zilizopo.


Amesema hata kampeni za kumsengenya zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa, kuponda huduma anayotoa zinalenga kushusha heshima na thamani yake aliyojenga kwa muda mrefu.


"Sitakubali na kuanzia kesho nazindua kampeni ya wiki mbili za kuwasha moto tutaona kama waumini watabaki katika makanisa yao," amesema.


Akihubiri leo Julai 14, 2024 katika ibada iliyofanyika kanisani kwake eneo la Buza Kwa Lulenge, amesema haiwezekani watu wakienda kusali kwao wanadai hawatapeliwi lakini wakienda kanisani kwake wanasema anatapeli waumini.


"Wote wanaonisengenya wana wivu kuna kitu hawana na wanatamani kufanya ninachofanya, wanaonisema vibaya wanasema hivi… sisi wenye Mungu wa kweli na tuna mafundisho ya kweli hatupati watu wakuwaambia, lakini huyu jamaa mjinga ana watu wengi,” amesema.


"Hicho ulichonacho unajuaje kama ni cha Mungu kwelikweli na kama kingekuwa cha Mungu kwelikweli basi watu wangewafuata. Nilisema waumini waliopo hapa ni walewale waliokuwa makanisani na misikitini juzi si jambo la kuficha nasema ukweli," amesema.


"Hakuna mchungaji, kanisa, msikiti wenye hakimiliki ya kumiliki watu… watu wako? Nasema hivi kama umekaa kwenye kanisa au msikiti kwa muda mrefu hujapona shida zako toka njoo hapa, ninawakaribisha waumini wa makanisa yote waje kusali hapa na msiwe na wasiwasi na wakikulaani na sisi tutawalaani hapahapa," amesema huku akishangiliwa na waumini.


"Kuna presha kubwa huko mitandaoni wachungaji wamekuwa wakali kwa waumini wao wakiwaambia kwamba yule mchawi msiende," amesema.


Amesema presha inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii haifanyiki kwa bahati mbaya, wanajua wazi katika kipindi kifupi kijacho yanaenda kuwa tupu.


Amewaeleza waumini anazindua kampeni ya wiki mbili kuanzia kesho, hivyo wajipange.


"Mtaelewa kwa nini wanalalamika wakienda kusali kwao hawatapeliwi mkija kusali hapa mnatapeliwa, mkienda kusali kwao mnaakili, lakini mkija hapa ninyi manyumbu haina shida bora uitwe nyumbu lakini uwe na hela," amesema.


Amewaeleza kabla ya kuwa nabii alikuwa mfanyabiashara na muumini wa kanisa moja eneo la Boko, jijini Dar es Salaam baadaye akaacha na kuanzisha kanisa hilo.


Mtume Mwamposa


Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Mtume Boniface Mwamposa amesema kuna makundi mawili yanayomfuatilia, wapo wanaomkubali kuwa ni mpaka mafuta na wengine wanatarajia akosee neno, ili wamuharibie kazi.


Akihubiri wakati wa ibada kanisani kwake eneo la Kawe amesema watu wanaomfuatilia wapo kwa ajili ya kusikiliza waone amekosea neno ili walipindue, walitumie kuharibu kazi ya Mungu anayoifanya.


"Soma maandiko acha kutafsiri sawasawa na wapinzani wa kazi ya Mungu, nazungumza na wanaonifuatilia si ninyi," amesema Mwamposa.


Amesema kazi anayoifanya si ya Mwamposa ni kazi ya Mungu aliye hai, hivyo wanatakiwa kufuata maandiko ya kitabu cha Biblia.


"Nataka nikupe siri, acha kujali watu wanaongea nini endelea na majukumu yako ya kazi, mipango yako na wao watakutafuta tu," amesema Mwamposa.


Amesema Biblia inasema: “Huyu ndiye akatuma mtu naye akamleta kwao naye alikuwa mwekundu mwenye macho mazuri na umbo lake la kumpendeza bwana akasema ondoka mtie mafuta maana huyu ndiye, ndipo Samwel akatoa pembe yenye mafuta akamtia mafuta kati ya ndugu zake na roho ya bwana ikamlilia Daudi kwa nguvu.”


Mwamposa amesema waelewe kanuni iliyopo kabla ya kumwagiwa mafuta, Mungu alikuwa mbali, lakini alipomwagiwa mafuta tayari roho ya kifalme ikashuka juu ya Daudi akaanza kufanya kazi, kutembea na kuwa na ufahamu.


“Someni Biblia mtaelewa mambo ya Mungu yapo wazi utachukua mafuta na maji ya upako utayaombea na kuachilia kwa watu, kisha wanapewa maelekezo aliyopewa na Mungu na si kuchanganya na kitu kingine,” amesema.


"Kuna mambo lazima uyaelewe watu wa giza wanachukua kitu hiki na kile wanachanganya, lakini hawa wana mambo mengi ya uharibifu. Ukija kwa Mungu kinachofanya kazi ni upako, ni nguvu ya Mungu na inafuatana na mafuta, kwa mafuta kiongozi wa kiroho amekwambia ufanye nini," amesema na kuongeza;


“Ukitaka ufaulu kaa chini ujifunze usililojua kwako ni usiku wa giza, sikiliza ujifunze mbona Mtume Buldoza yupo kwenye runinga na redio, wapo watu wanasema hawataki kumsikiliza wamekosa hekima wanatakiwa wasibishane na kitu ambacho hawajakisikiliza kimaandiko halafu wajue cha kufanya.


Amesema wapo baadhi ya Watanzania wamemkataa, lakini watu kutoka mataifa mbalimbali kama Ubelgiji, Uganda, na Uholanzi wamekuja nchini kupokea uponyaji na wanamuamini.


Nabii Suguye


Muumini katika Kanisa la World of Reconciliation Ministry (WRM) lililo chini ya Nabii Nicholaus Suguye alikana kupangwa watu wa kutoa shuhuda.


Amesema hayo baada ya Nabii Suguye kumsimamisha, Upendo Nassari ambaye awali alitoa ushuhuda kanisani hapo akieleza kuponywa ugonjwa wa figo uliomsumbua kwa miaka 11.


Suguye alipoingia kuhubiri, aliomba kumuona Upendo akasema: “Nilikuwa namkagua macho yake ni haya kweli (namna yalivyokuwa yamevimba awali na yalivyo sasa), ikifika hali kama hii wakati mwingine wazoefu wa changamoto za figo wanasema hapa tunamsubiri bwana.”


Ndipo muumini mwanamume alimsogelea na alipopewa kipaza sauti alisema: “Watu si waone makaratasi haya sasa, ili waseme baba anapanga watu hapa, dunia ione hayo makaratasi kwa sababu mimi niliambiwa nilipangwa nilipopona Ukimwi mwaka 2016 sasa haya makaratasi dunia ione.”


Katika hilo, Suguye amewataka waumini wafahamu kile Mungu anachokifanya ndani ya kanisa hilo, akieleza hawampigi mtu picha kwa ujanja kwa kumfichaficha.


“Sijui afichwe huku, afichwe huku, avishwe baibui, tunaonyesha, ili baadaye fuatilia mwenyewe uone kile ambacho nabii anachokifanya halafu uliza hao ambao wanafanyiwa hapa wamelipa nini,” amesema.


Suguye amesema kwa miaka yake yote anayotumika mbele za Mungu amekuwa akifanya huduma na anapendelea zaidi maombezi kwa wote kama ilivyo ibada ya leo Julai 14, 2024 ambayo waumini wote watawekewa mikono na watafunguliwa.


“Ukichukua hela hovyo ugonjwa ni roho, ile roho inaweza kuhama yote ikaingia kwako, ni vile watu tu ambavyo hawana ufahamu wa kiroho sawasawa,” amesema.


Amesema unapomuombea mtu kwa roho nyeupe bila kuhitaji chochote Mungu humuongezea maisha marefu.


Mzee wa Upako


Mchungaji Antony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako wakati wa ibada amewakosoa wanaompinga kwa maneno yake ya kimungu.


Katika ibada amewaahidi waumini wake wote watakuwa matajiri, lakini waongeze jitihada katika kufanya kazi zao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad