Mfahamu Manji Kwa Undani, Mchango Wake Katika SOKA la Bongo..Hakika Yanga Hawata Msahau Kamwe

Mfahamu Manji Kwa Undani, Mchango Wake Katika SOKA la Bongo..Hakika Yanga Hawata Msahau Kamwe

MWENYEKITI na mfadhili wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji amefariki dunia jana baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Manji amekutwa na umauti huo Juni 29, 2024 akiwa jijini Florida, Marekani, akiwa anapatiwa matibabu.

Bado familia ya Manji haijaweka wazi kilichokatisha uhai wa bilionea huyo, ingawa taarifa za kifo chake zimethibitishwa na mtoto wake wa kiume Mehbub Manji.

“Ni kweli baba amefariki jana usiku saa sita, akiwa hapa hospitalini, akipatiwa matibabu,” alisema Mahboub akizungumza na gazeti la Mwanaspoti kwa kifupi huku akiwa kwenye majonzi makubwa.

Hapa nchini Manji alikuwa na jina kubwa, akiwa mfanyabiashara tajiri lakini pia aliwahi kuiongoza Yanga kwa mafanikio.

Manji aliipa nguvu kubwa Yanga akiwa kama mfadhili lakini pia baadaye akaongoza kama mwenyekiti ikiwa timu tishio hapa nchini na nje ya Tanzania.

Mara ya mwisho Manji kuonekana kwenye shughuli ya Yanga ni pale alipokuwa sehemu ya watazamaji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiichapa Simba kwa mabao 2-1, Aprili 20, 2024.

MANJI NI NANI?

Yusuf Manji alianza kufahamika vizuri nchini na Afrika kwa ujumla baada ya kuchukua biashara za baba yake mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 20 tu na kuzisambaza duniani kote kwa kutengeneza utawala mkubwa wa Quality Group Limited.

Alijulikana zaidi kwa kuleta Tanzania majina makubwa ya biashara kama General Motors, ISUZU, Mahonia, Hertz na Bridgestone.

Kampuni zake zimefanya biashara ya mazao ya baharini na ziwani na zaidi ya makampuni 30 barani Asia na Ulaya, pia ikijenga majengo makubwa ikiwamo mall ya kwanza ya kisasa ya Quality Center na pia amezalisha mchele kwa njia za kisasa.

KUTUA YANGA

Manji aliingia Yanga kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika Juni, 2012 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga kujiuzulu mara kutokana na shinikizo lililoibuka kufuatia timu hiyo kufumuliwa mabao 5-0 na Simba katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Mei 6, 2012 Kwa Mkapa.

Kuingia kwa Manji kuliifanya Yanga kuwa tishio nchini kwa kuweza kuzoa mastaa kadhaa kutoka klabu mbalimbali za nchini na zile za kimataifa na kuifanya itambe Afrika.

Miongoni mwa wachezaji walionyakuliwa kwa nguvu na fedha za Manji ni aliyekuwa beki tegemeo wa Simba, Kelvin Yondani, kipa Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Hassan Ramadhan Kessy na kubwa ni namna alivyomteka Mbuyu Twite aliyekuwa akielekea mikononi mwa Simba.

Wakali wengine aliowaleta na kuifanya Yanga kuwa tishio ikiwamo kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2016 na kurudia tena 2018 ni pamoja na Donald Ngoma, Amissi Tambwe aliyetoka Simba, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa, Thabani Kamusoko na wengine.

Pia alihusika kuleta makocha wa maana na wenye majina makubwa kama Ernie Brandts, Tom Saintfiet, Hans Van Pluijm, Marcio Maximo na George Lwandamina aliyekuwa wa mwisho chini ya Manji kabla ya bilionea huyo kutangaza kujiuzulu Mei 22, 2017.

Akiwa Mwenyekiti wa Yanga, aliiwezesha Yanga kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara misimu minne tofauti ukiwa ule wa 2012-2013 na ile mitatu mfululizo ya 2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017, mbali na Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Kagame 2012 lililokuwa la mwisho kwa klabu hiyo.

Manji alijiuzulu nafasi hiyo Mei 22, 2017 baada ya kuiwezesha Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo, jambo lililoifanya klabu hiyo kuyumba kiasi cha kutembeza bakuli lililohamasishwa kwa jina la Kubwa Kuliko.

Sababu ya kujiuzulu kwa Manji kwa kipindi hicho ilitokana na kuzozana na Wazee wa Yanga na baadhi ya wanachama wakiongozwa na Ibrahim Akimali ‘Roman Abramovich’ waliokuwa wakipinga mpango wake wa kutaka kukodishwa klabu hiyo.

Miezi michache tangu alipojiuzulu Uenyekiti wa Yanga, Manji akiwa Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu alitangazwa kuvuliwa nafasi hiyo Septemba 2017, kisha kuingia kwenye misukosuko ya kufunguliwa kesi zilizomfanya baadaye kuamua kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini na baadaye Marekani.

Mwaka 2021 alirejea nchini na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Yanga na kuibua tetesi kwamba alikuwa akijiandaa kurejea klabuni kabla ya kuondoka zake na Aprili mwaka huu gazeti la Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu naye, yaliyokuwa ya kwanza na mwisho kwake kabla ya mauti kumkuta usiku wa jana huko Marekani.

WADAU WAMLILIA

Akizungumzia kifo hicho, nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema amesikitishwa na taarifa hizo huku akiweka wazi Manji atabaki katika mioyo ya timu hiyo, kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya baada ya kupitia kipindi kigumu.

“Ni taarifa ya huzuni sana kwa wanamichezo kwa sababu Manji aliandika historia ya kuifanya Yanga kuwa timu tishio, kwa sababu kama unakumbuka kabla ya kuingia kwake madarakani, ilipitia changamoto kubwa ya kuandamwa na ukata.”

Chambua aliongeza, atamkumbuka Manji kwa mengi hasa nia yake ya kutaka kumfundisha ukocha katika nchi ya England kipindi akiwa Yanga.

“Yanga nimeitumikia kwa miaka 14, 10 nikiwa kama mchezaji na minne nikiwa kama kocha, nakumbuka alitaka kunipelekea nchini England kwa ajili ya masomo zaidi ya ukocha, japo sikufanikiwa hilo ila namkumbuka kwa moyo wake mzuri juu yangu.”

Kwa upande wa Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema, amesikitiswa zaidi na kifo cha Manji, kwani licha tu ya upinzani wa timu walizoziongoza au kuzishabikia, walikuwa ni miongoni mwa marafiki waliokuwa wanaheshimiana.

“Alikuwa mtu mcheshi na asiyekuwa na makuu, nakumbuka wakati wa uongozi wetu, nililazwa Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, kwa bahati nzuri na yeye alikuwepo hivyo tukawa chumba kimoja, kiukweli nimeumia baada ya kusikia taarifa hiyo.”

Credit:- MwanaSpoti

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad