Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, mganga wa jadi, Nikas Nazario, baada ya kumtia hatiani kwa mauaji ya Livence Kalindo, aliyempiga risasi akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.
Miongoni mwa mashahidi wa upande wa mashtaka alikuwa mke wa mshtakiwa.
Mauaji yanadaiwa kufanyika Agosti 5, 2020 katika Kijiji cha Katapulo, wilayani Kalambo mkoani Rukwa.
Hukumu hiyo ambayo ipo katika mtandao wa mahakama, imetolewa Julai 12, 2024 na Jaji Deo Nangela, aliyesikiliza kesi hiyo, ambaye ameeleza ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka, hivyo kumtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
Siku ya tukio saa mbili usiku ilidaiwa kutokea mlipuko kwenye kituo cha biashara kijijini hapo, jengo ambalo lilikuwa linamilikiwa na watu wawili, Agusta Maluko (mke wa mshtakiwa) aliyekuwa akiuza nyama choma na mwenzake akiuza pombe ya kienyeji.
Kutokana na mlipuko, waliokuwapo walitawanyika, lakini muda mchache baadaye ilibainika Kalindo ameuawa kwa kupigwa risasi.
Baada ya uchunguzi wa polisi mshtakiwa alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane, wa kwanza akiwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Nikas Katewa, aliyedai alipokea simu na alipofika eneo la tukio alimtambua marehemu kwa sura akivuja damu jirani na shingo.
Alitoa taarifa Kituo cha Polisi Matai, askari walipofika waliukuta mwili, kisha walienda kwenye nyumba ya Agusta ambako hakukuwa na mtu. Mshtakiwa alikamatwa kwenye Kijiji cha Kasakamulo nchini Zambia.
Alidai Agosti 6, 2020 akiwa na mmoja wa ndugu wa marehemu walienda Hospitali ya Rufaa ya Sumbawanga kushuhudia uchunguzi wa mwili.
Shahidi wa pili, Agusta ambaye ni mke wa mshtakiwa kabla ya kutoa ushahidi kwa mujibu wa kifungu cha 130 (1) cha Sheria ya Ushahidi, baada ya kujua haki zake chini ya sheria, alikuwa tayari kutoa ushahidi dhidi ya mumewe, akisema hakuna mtu aliyemlazimisha kufanya hivyo.
Alidai alimfahamu Kalindo kwa kuwa alikuwa akiishi kijijini hapo ila hakuwa na uhusiano naye.
Shahidi alidai siku ya tukio alisikia mlipuko wa kitu kama vile bunduki na wakati huo, kulikuwa na watu wengi kwenye baa. Alidai baada ya mlipuko Kalindo alianguka na alikuwa akivuja damu kichwani.
Alidai alifunga biashara na kurudi nyumbani na hakujua mume wake alikuwa wapi, lakini alipofika alimkuta ameketi akamwambia waondoke.
Shahidi alidai alipomweleza kuna mtu ameuawa ndiyo sababu ya yeye kurudi nyumbani, mshtakiwa hakusema lolote.
Alidai waliondoka kuelekea Zambia kwa miguu usiku huo kwa kutumia njia zisizo rasmi (za msituni) na kwamba walilala kwenye kambi iliyopo msituni mbali na kijiji, kisha wakapanda mashua asubuhi kwenda Zambia ambako walikaa kwa muda wa wiki tatu, kabla ya mumewe kukamatwa.
Alidai alipomuuliza mume wake amefanya nini alimjibu "Mmh! ni mimi nimefanya hicho kitendo cha kumpiga risasi Livence Kalindo."
Alidai baada ya kauli hiyo mumewe alinyamaza.
Shahidi alidai mume wake alikuwa mganga wa jadi akifanya shughuli za uganga nchini Zambia na kwamba, hakuona mume wake akimpiga risasi Kalindo siku ya tukio.
Alikiri mumewe alikuwa akitembelea Zambia kwa shughuli za biashara na wakati mwingine hukaa huko kwa muda mrefu.
Shahidi wa nne, Giles Nazario, ambaye ni ndugu wa mshtakiwa alidai siku ya tukio baada ya kusikia mlipuko kama wa tairi kupasuka alikwenda kulala kwenye shamba lake kwa kuwa aliogopa kukamatwa na polisi.
Alidai alikutana na mshtakiwa na mkewe wakiwa wamebeba ndoo yenye nyama ya mbuzi na alipowauliza wanaelekea wapi, walimwambia: “Huko tulikotoka kumechafuka, kwa hiyo walikuwa wakienda kuacha nyama nyumbani kwa mwanaye kisha waondoke.”
Alidai mshtakiwa alikuwa akivuta mkono wa mkewe kwani alisita kumfuata.
Alidai hakuona mshtakiwa akimuua Kalindo ila siku ya tukio alikutana na mshtakiwa na mkewe wakikimbia.
Shahidi wa sita ambaye ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Matai, Elias Mkama akiwa mlinzi wa amani, Septemba 8, 2020 alirekodi ungamo la mshtakiwa.
Alidai alimweleza haki zake kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na haki ya kukaa kimya au kunyamaza na kuwa alirekodi maelezo ya mshtakiwa na baada ya kumsomea, alithibitisha kuwa kilichorekodiwa ni sahihi kwani alikieleza.
Shahidi huyo aliwasilisha taarifa hiyo mahakamani na kueleza mshtakiwa alikiri kumuua Kalindo.
Kwa mujibu wa mshtakiwa alikamatwa saa moja asubuhi Septemba 4, 2020 na mauaji yalifanyika saa 7.45 mchana.
Alidai mshtakiwa alimweleza sababu za mauaji ni mbili, tuhuma za uchawi akidai alikuwa akiroga ng'ombe wake, na pili ni wivu.
Shahidi wa saba, daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alieleza aliona upande wa kulia wa fuvu ulikuwa umevunjika, na shingoni aliona matundu mawili.
Kwa mujibu wa uchunguzi kifo kilitokana na kuvuja damu nyingi kichwani na kwenye ubongo.
Shahidi wa nane, ambaye ni ofisa wa polisi alidai walipofika kijijini walielezwa mshtakiwa ndiye muhusika wa tukio hilo kwa kuwa alikuwa akimtuhumu marehemu kwamba anamroga na alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mkewe.
Alidai mshitakiwa alikamatwa baada ya Polisi wa Zambia kuwaeleza wenzao wa Tanzania kuwa wamemkamata na alikuwa Kituo cha Polisi cha Mpulungu kwa tuhuma za kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Alidai wakati wa mahojiano mshtakiwa alimwambia yeye ndiye mhalifu aliyemuua kwa kumpiga risasi Kalindo kwa sababu alikuwa akiiroga familia yake na kuwa na mapenzi na mke wake.
Utetezi wa mshtakiwa
Akijitetea mahakamani, mshtakiwa alidai ni mkulima anayefanya biashara kati ya Tanzania na Zambia na ufukweni mwa Ziwa Tanganyika.
Alidai siku hiyo mkewe alienda eneo lake la biashara na baadaye alirudi nyumbani akikimbia akimweleza kuna kitu kililipuka mithili ya tairi la pikipiki na mtu akaanguka na kulala chini.
Mshtakiwa alieleza mahakama alimshauri mkewe waondoke haraka kwani kulikuwa na uwezekano kuwa angehojiwa juu ya jambo hilo ambalo hakuwa na habari nalo.
Alidai mkewe alikwenda kwa ndugu zake Kijiji cha Kisumba, na yeye kuelekea Zambia.
Alidai waliondoka kwani kuna tabia katika kijiji hicho kwamba kila linapotokea tukio baya Polisi wanaenda kutesa watu.
Alidai alikamatwa na Polisi wa Zambia kwa sababu hati yake ya kusafiria ilikuwa imeisha muda wake na kuwa alipokuwa anahojiwa kituo cha polisi alitaka ndugu au mwenyekiti wa kijiji awepo.
Alidai Polisi walimtesa, kumfunga pingu na kumpiga kwa rungu, akiachwa akining'inia kwenye chuma kwa lengo la kumlazimisha kuwaambia ukweli. Pia alipelekwa kwa hakimu akiambiwa akiri kosa hilo.
Alikana kumfahamu Kalindo wala kumuua na hakuwahi kumweleza mkewe kuwa yeye alihusika na kifo hicho.
Alidai alisafiri hadi Zambia kwa basi liitwalo Kambole Express na kulipa nauli Sh3,000 na baadaye alitembea kwa miguu kuvuka mto Kalambo bila kuonana na polisi wa mpakani na kudai ameshindwa kumwita mke wake wa pili kama shahidi wake kwa sababu hakujua lolote kuhusu kesi iliyokuwapo.
Hukumu ya mahakama
Jaji alieleza katika kesi ya jinai mzigo wa kuthibitisha kosa unabaki upande wa mashtaka bila kuacha mashaka yoyote.
Alieleza katika kesi iliyopo mbele yake hakuna ubishi kwamba Kalindo amefariki dunia na kwamba, kifo chake hakikuwa cha kawaida na suala ya kujibiwa na kuthibitishwa pasipo shaka yoyote ni iwapo mtuhumiwa ndiye aliyehusika.
“Ipo haja ya kuangalia mazingira yote ya kesi hiyo, kwani hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja kwamba mshitakiwa alionekana akimpiga risasi marehemu, kwa hiyo, kesi hiyo imeegemezwa kwenye ushahidi wa kimazingira,” alieleza Jaji.
Alisema mshtakiwa na mkewe (shahidi wa pili) walikiri kuondoka kwenda Zambia baada ya mauaji kutokea na kuwa kwa ushahidi uliotolewa na shahidi wa kwanza, pili, nne, nane na mshtakiwa mwenyewe zinajumuisha ushahidi wa mwenendo.
Alieleza bado kuna ushahidi mwingine unaostahili kuzingatiwa, ambao ni wa shahidi wa sita na maelezo ya ziada ya mahakama ya mshtakiwa ambayo yalirekodiwa na shahidi huyo ambayo yanaonyesha alikiri.
“Ninapotazama ukurasa wa sita wa kielelezo cha pili, yafuatayo ni maneno kamili ambayo mtuhumiwa aliyasema mbele ya mlinzi wa amani (hakimu) na ambayo kisheria yanajumuisha ungamo. Nanukuu kwa Kiswahili:
"...Tarehe 05/08/2020 ndipo nilipomkuta na mke wangu nje ya baa ya Kantongama wakilishana nyama, ndipo hasira ikanipanda, ndipo nikamuua kwa bunduki aina ya Griner iliyoletwa kwangu kwa ajili ya marekebisho hapo nyumbani, na muda huo nilipomuua ilikuwa saa mbili kasoro usiku."
Akinukuu rufaa ya jinai namba 176/2017 ya Machi 30, 2020 katika Mahakama ya Rufani katika kesi ya Geofrey Sichizya dhidi ya DPP, maneno yaliyosemwa na mshtakiwa yanajumuisha kuungama.
Jaji alisema kutokana na uchambuzi wa ushahidi uliotolewa, ingawa hakuna shahidi wa moja kwa moja aliyemwona mshtakiwa akitenda kosa hilo, maungamo yake ya mdomo na kuthibitishwa na shahidi wa pili na kwa kuzingatia mwenendo wake baada ya kutenda kosa, yanahitimisha alimuua Kalindo.
“Kwa kuwa mahakama hii imemkuta mshtakiwa Nikas na hatia ya kosa linalomkabili na hivyo kumtia hatiani, natoa hukumu hii, mshitakiwa atauawa kwa kunyongwa kama ilivyoelezwa chini ya kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,” alihitimisha Jaji.