Dar es Salaam. Kutenguliwa ni jambo moja, lakini kutenguliwa ukiwa katikati ya shughuli za nafasi uliyotenguliwa kwayo ni jambo lingine, hiki ndicho kilichomkuta aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye si mara yake ya kwanza.
Taarifa ya kuondolewa kwa Nape katika wadhifa huo ilitolewa jana Jumapili Julai 21, 2024, akiwa katikati ya hotuba kwenye hafla ya utoaji tuzo za wanawake wa kidigitali zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambako alikuwa mgeni rasmi. Shughuli hiyo ilikuwa ikirushwa mubashara na kituo cha televisheni cha TV E.
Baada ya taarifa za kuondewa kwenye wadhifa huo, mbunge huyo wa Mtama (CCM), Mkoa wa Lindi amesitisha kwa muda akaunti yake kijamii ya X (zamani Twitter). Kusitisha kwake, kumeibua mijadala ya kumsaka na kuhoji imekuwaje.
Katika mtandao wa X, Nape ndiyo miongoni mwa maeneo aliyokuwa akitumia kuwasilishana na kuchangia mijadala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Hii ni mara ya pili kwa mwanasiasa huyo anakumbwa na utenguzi katika mazingira yanayofanana, aliwahi kuondolewa katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo akiwa katika harakati za kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda ya kuchunguzi tukio la uvamizi wa kituo cha redio cha Clouds mwaka 2018.
Safari ya Nape katika wadhifa wa uwaziri ilianza mwaka 2015 baada ya Rais wa wakati huo, John Magufuli alipomteua kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na miaka miwili baadaye alimuondoa.
Hakukuwa na sababu iliyowekwa wazi na mamlaka ya uteuzi juu ya kuondolewa kwake, isipokuwa wengi walihusisha na uamuzi wake wa kuunda kamati ya uchunguzi dhidi ya uvamizi wa kituo cha redio cha Clouds.
Nape aliondolewa siku aliyokuwa anapokea ripoti ya kamati hiyo iliyomtuhumu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutumia vibaya mamlaka yake kwa kuvamia kituo hicho cha redio.
Mara ya pili, aliteuliwa tena kushika wadhifa wa uwaziri mwaka 2022, wakati huo akiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, amedumu ndani ya wizara hiyo kwa miaka miwili pekee na jana usiku wa Julai 21, 2024 aliondolewa bila kuelezwa sababu yoyote.
Lakini kuondolewa kwake wakati huu kunahusishwa na kauli aliyotoa hivi karibuni iliyoibua mijadala katika mitandao ya kijamii, kuhusu ushindi wa uchaguzi nje ya boksi la kura.
“Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe,” alisema Nape Julai 15, 2024, akiwa mkoani Kagera.
Pamoja na kupingwa mitandaoni, kauli hiyo ilipingwa pia na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla aliyesema si msimamo wa chama hicho.
“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambie hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” alijibu Makalla alipokuwa ziarani mkoani Dar es Salaam.
Mtazamo wa kisiasa
Akizungumzia uamuzi wa kuondolewa kwa Nape, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema pengine kauli yake ya Julai 15 ndiyo iliyomponza.
“Yalikuwa makosa makubwa kwa kiongozi mwandamizi kama Nape kutoa kauli kama hizo zenye kukichafua chama (CCM) na Serikali juu ya uchaguzi.
“Kauli yake inaweza kuwa imechukuliwa kama uthibitisho kwa wapinzani ambao mara zote wamekuwa wakilalamika kuibiwa kura,” ameeleza.
Dk Kabobe amehusisha kuondolewa kwa Nape na madai yaliyowahi kutolewa na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akimtuhumu kwa hujuma za uchaguzi ndani ya CCM wakati wanapiga kura za kuwachagua wabunge wa Afrika Mashariki (EALA).
“Ukizingatia kuwa Rais anatekeleza vizuri falsafa yake ya 4R, vitendo kama hivi vya kumrudisha nyuma lazima avikemee na kulinda chama na Serikali yake kwa wivu mkubwa. Nadhani hiki ndo alichokifanya,” amesema.
Kwa kuwa mwaka huu na ujao kuna chaguzi, Dk Kabobe amesema kauli kama hizo hazipaswi kufumbiwa macho na ndio maana mamlaka ya uteuzi imeonyesha njia na inastahili pongezi kwa hilo.