Mabosi wa Simba wanaendelea kushusha mashine mpya kwa ajili ya kutengeneza kikosi cha msimu ujao, lakini kiungo nyota wa timu hiyo, Fabrice Ngoma ameshindwa kujizuia akisema kwa aina ya wachezaji wanaotua Msimbazi anaona kabisa msimu ujao Wekundu hao wakirejesha mataji waliyoyapoteza kwa Yanga.
Ngoma amesema kinachompa jeuri ya kuitabiria Simba kubeba ndoo ilizozitema kwa Yanga kwa misimu mitatu mfululizo ikiwamo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho ni kutokana na wachezaji wanaosajiliwa kuwa na umri mdogo unaowapa nafasi ya kufanya mambo kulinganisha na kikosi cha Simba kilichopita.
Hadi sasa Simba imewatambulisha Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya Zambia, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana, Lameck Lawi (18) kutoka Coastal Union, huku ikihusishwa na majembe mengine yenye wastani wa umri usiozidi 28.
Ngoma alisema akiangalia umri wa wachezaji hao anaona wengi watakuwa na njaa ya kupambania mafanikio na kutengeneza wasifu wao, hivyo wakiungana na wazoefu anaamini Simba itafanya mambo makubwa msimu ujao.
“Nimeona wachezaji ambao klabu imewatangaza. Binafsi inanipa moyo kuuona msimu ujao utakuwa zamu yetu kunyakua mataji kama ya Ligi Kuu Bara, FA na mengine ambayo tuliyakosa msimu uliopita,” alisema Ngoma aliyetua msimu uliopita kutoka Al Hilal ya Sudan na kuongeza:
“Ukiachana na umri wao kiufundi ni wachezaji wazuri, ndio maana Simba ikawapa nafasi ya kuja kutumika ndani ya kikosi chao.”
Ngoma ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao matatu katika Ligi Kuu, alisema kikosi kikiwa na mchanganyiko wa umri, anaona kinakuwa na ushindani mkali na uhakika wa kushinda mechi.
“Binafsi nawakaribisha ili tuendelee kuifanya kazi ya Simba na kuwapa furaha mashabiki wetu, ambao wana hamu kuona tunachukua mataji,” alisema Ngoma ambaye mapumziko yake aliyatumia kukaa kwa muda mrefu na familia yake.
AUCHO AMCHAMBUA MUKWALA
Kiungo mkabaji wa Yanga, Khalid Aucho alisema kwa uwezo anaoujua wa mshambuliaji Mukwala anaiona Simba inakwenda kufaidika na huduma yake.
“Kwanza namkaribisha katika Ligi Kuu ya Tanzania. Atahitajika kupambana. Kuhusu uwezo wake ni mzuri na naamini ataifanyia mambo makubwa Simba,” alisema Aucho.