Kama ambavyo awali Mwanaspotui liliwajulisha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua alipewa siku tano kushughulikia pasipoti yake kabla ya kuungana na wenzake kambini Afrika Kusini, taarifa zikufikie nyota huyo tayari ameshatua huko na keshokutwa huenda akacheza dhidi ya Kaizer Chiefs.
Awali Mwanaspoti lilipata taarifa, huenda Pacome angekuja moja kwa moja jijini Dar es Salaam kutoka Ivory Coast alipoenda kushughulikia hati hiyo ya kusafiria wakati wenzake wakienda Sauzi, lakini ghafla leo mchana ikaelezwa viongozi wamekubaliana na kocha Miguel Gamondi aende huko huko.
Kocha Gamondi alisema alipanga Pacome atangulie Dar es Salaam kisha kuandaliwa mazoezi ya ziada ili kwenda sambamba na wenzake, lakini muda umeonekana na ni mdogo hivyo kutakiwa atue Sauzi kabisa jana mchana ili aungane na timu kujiandaa na mechi ya kesho ya Kombe la Toyota dhidi ya wenyeji Amakhozi.
“Pacome yupo hapa Afrika Kusini, ameshaungana na wenzake kwa ajili ya mechi ya Jumapili dhidi ya Kaizer Chiefs, kisha tutarudi wote kuendelea na maandalizi ya mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki katika Tamasha la Yanga na baadae mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Tulikuwa tukutane naye Dar na nilishamwandalia mazoezi maalumu aliyotakiwa kuyafanya baada ya kukosa mechi mbili za awali za kirafiki zilizochezwa Mpumalanga na angekuwa sawa tu na wenzake kwa upande wa utimamu wa mwili, ila muda ungekuwa mdogo kwa kazi iliyopo mbele yetu, ndio maana ameunga huku.”
Gamondi alisema licha ya kukosa mazoezi na mechi hizo za awali huko Sauzi, bado anaamini ni mchezaji aliye makini na hatakuwa na utofauti na wenzake, hivyo kukosekana kwake kwa hapo awali kusiwape tabu mashabiki wake hakuna kitakachopungua kwa upande wa mchezaji huyo.
Pacome alikosa mechi dhidi ya Augsburg ya Ujerumani ambapo Wananchi walilala kwa mabao 2-1, kisha kushinda bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa michuano ya kimataifa ya Kombe la Mpumalanga, TS Galaxy ya huko.
Kesho Yanga itashuka tena uwanjani kuvaana na Kaizer Chief ya mjini Johannesburg katika mechi ya Kombe la Toyota, huku ikiwakutanisha na aliyewahi kuwa kocha wa kikosi hicho cha Jangwani, Nasreddine Nabi aliyetua Kaizer akitokea FAr Rabat ya Morocco.
Baada ya mechi hiyo, Yanga itarudi kujiandaa na Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 4 kabla ya kucheza na Simba katika Ngao ya Jamii kuzindua msimu mpya wa 2024-2025 siku ya Agosti 8 na atakayeibuka mbabe atacheza na mshindi wa mechi kati ya Azam FC na Coastal Union, Agosti 11