Siku moja tu baada ya mabosi wa Yanga kutoa tamko juu ya hukumu ya kesi iliyofunguliwa na wanachama wa klabu hiyo kulikataa Baraza la Wadhamini na kuweka rehani nafasi za viongozi waliopo madarakani, Waziri mwenye dhamana na michezo, Dk Damas Ndumbaro ameamua kujitosa katika sakata hilo.
Dk Ndumbaro ambaye ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema njia sahihi kwa Yanga kutatua migogoro na wanachama wake ni kukaa meza moja na kufikia muafaka.
Ndumbaro amesema hayo baada ya mgogoro baina ya wanachama wa klabu hiyo na viongozi kutokana na hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Agosti 2, 2023 ambayo imeuondoa madarakani uongozi wa sasa.
Hukumu hiyo inatambua Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1968 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2011.
“Mimi niwashauri viongozi na wanachama wa Yanga, migogoro haina tija na inarudisha nyuma maendeleo. Pia inawaondoa katika ‘reli’ ya kufanya maandalizi ya timu yenye jukumu kubwa la kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa ya CAF),” alisema Waziri huyo na kuongeza;
“Nawashauri wakae meza moja na kutatua, endapo kila mmoja atakuwa anazungumzia kona yake, itachukua muda kumaliza. Wanachotakiwa sasa ni kufanya mjadala wa pamoja na wajue namna ya kumaliza changamoto hiyo. Hii ndiyo njia bora na sahihi zaidi.”
Waziri huyo ambaye ni Mwanasheria pia, aliwakumbusha viongozi wa Yanga na klabu nyingine kufuata taratibu za kisheria wanapofanya mabadiliko ya uongozi kwa mujibu wa katiba.
“Pia viongozi wanatakiwa kufuata sheria, kanuni, taratibu au maagizo yaliyowekwa (Compliance). Ni wakati wa klabu kufanya kazi zake kwa kufuata masharti na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika. Ni muhimu kwa viongozi wa klabu zote. Hii itasaidia kuondoa matatizo kama haya,” alisisitiza Ndumbaro.
Alisema taratibu zipo wazi, lakini inaonekana kufuatwa inakuwa shida, jambo linalotoa mwanya kwa watu wengine kufanya wanayoona yanafaa.
Kwa sasa, uongozi wa Yanga unasubiri maamuzi ya mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu baada ya kuwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kufanya mapitio ya kesi ambayo maamuzi yake yanauondoa uongozi wa sasa madarakani.
Mkurugenzi wa Sheria wa klabu hiyo, Simon Patrick alisema wamechukua hatua hiyo kutokana na ukweli hawakujua kufunguliwa kwa kesi hiyo hadi kuamuliwa kwake na baada ya kukubaliwa ombi lao, pia watawasilisha maombi ya kufanya marejeo ya kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na Juma Ally na Geofrey Mwaipopo dhidi ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.