Klabu ya Coastal Union imesema inausubiri Uongozi wa Simba wakae meza moja kulimaliza pembeni sakata la usajili wa beki Lameck Lawi ambaye shauri lake lilikuwa kkamati ya usuluhishi ya TFF.
Ikumbukwe baada ya Simba kupeleka malalamiko yao kwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juu ya sakata hilo la usajili.
Klabu hizo zilitakiwa kukaa meza moja na kumalizana juu ya usajili wa mchezaji huyo ambaye Simba wanadai wamemsajili kihalali huku Coastal Union wakikana kwa kile wanachodai wenzao hao hawakufuata makubaliano yao.
Msemaji wa Coastal Union, Abbas El Sabri, alisema jana kuwa wao wanawasubiri mezani Simba kama walivyoshauri kamati hiyo ya TFF.
“Ni kweli tulipewa ushauri huo, sisi hatuna shida tunawasubiri wenzetu wa Simba watakapokuwa tayari tukutane kulimaliza suala hili, kama tulivyosema awali sisi hatua shida, Simba wakiwa tayari tutaenda kukutana nao,” alisema El Sabri.
Hata hivyo, El Sabri alikiri licha ya mchezaji huyo kumworodhesha kwenye usajili wao msimu ujao, kwa sasa yupo nje ya nchi kwa mambo yake binafsi.
“Lawi yupo Ubelgiji kwa mambo yake binafsi, lakini ni mchezaji wa Coastal na tumepeleka jina lake CAF kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo tutashiriki msimu ujao,” alisema El Sabri.
Kwa upande wake, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa na uongozi wa juu wa klabu hiyo.
“Kama kutakuwa na lolote wana Simba watafahamu, kwa sasa suala hilo lipo ngazi ya juu na limefika TFF, mbivu na mbichi zitajulikana hapo pande zote zitakapokutana,” alisema Ahmed.