Klabu ya Simba imefunguka kuhusu wachezaji wao wawili, kipa Aishi Manula pamoja na beki wa pembeni, Israel Patrick Mwenda kutofika kambini nchini Misri mpaka sasa licha ya kuwa na mikataba na klabu hiyo.
Ahmed amesema hayo ikiwa ni wachezaji wanne sasa wa Simba ambao hawajafika kambini zikiwa zimepita wiki mbili tangu timu hiyo itue Ismailia kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
“Aishi Manula pamoja na Israel Mwenda wote bado hawajajiunga na kambi lakini hao wote sina majibu ya moja kwa moja kwamba ni kitu gani kinawafanya wasijunge na kambi, nitakapopewa taarifa rasmi nitawapa taarifa Watanzania nini kinaendelea juu yao.
“Hakuna changamoto hata kidogo, tuko imara na madhubuti mno, wachezaji wote ambao hawajawasili kambini mpaka sasa hawatuathiri hata kidogo, maandalizi yetu tunayoyafanya yamekamilika kwa asilimia zaidi ya 100.
“Hawa wachezaji ambao hawapo kambini kutokuwepo kwao hakutuathiri hata kidogo, ni kama kachumbari tu kwenye pilau. Wachezaji 29 wapo kambini nchini Misri, ni vikosi viwili kamili na unapata wachezaji wa akiba kwa hiyo tuko madhubuti,” amesema Ahmed.
Wachezaji wa Simba ambao hawajafika kambini mpaka sasa ni;
Israel Mwenda (Hajatoa taarifa)
Aishi Manula (Hajatoa taarifa)
Kibu Denis (Mgomo baridi)
Aubin Kramo (Anatafutiwa timu kwa mkopo)
Lameck Lawi (Usajili wake una sintofahamu ambapo TFF imezitaka Simba na Coastal Union kumalizana kwa busara).