Sugu Ampiga Dongo Msigwa Kutimkia CCM

 

Sugu Ampiga Dongo Msigwa Kutimkia CCM

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa kimesema kuondoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wa kanda hiyo, Mchungaji Peter Simon Mgwa hakuathiri chochote katika chama hicho, kwa sababu chama hicho ni jeshi kubwa la watu wenye uwezo wa kukiongoza.


Hayo yamebainishwa Julai 12, 2024 mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu wakati wa kikao cha baraza la mashauriano la chama hicho.


Mchungaji Msigwa alihama Chadema kwenda CCM, Juni 30, 2024 ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa kanda ya Nyasa, ambapo Sugu aliibuka mshindi kwenye uchaguzi huo wa ndani ya chama.


Hata hivyo, Msigwa alilalamikia matokeo hayo akidai kwamba alihujumiwa na kupokwa ushindi wake, kutokana na kile alichodai ni maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa chama hicho, jambo ambalo alilikatia rufaa kabla ya kutimkia CCM.


Akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo, Sugu amewataka wanachama na viongozi wa Chadema katika kanda hiyo, kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na badala yake waungane kuwa kitu kimoja, ili washiriki katika kukijenga chama kuelekea chaguzi.


“Tuna ajenda ya kwenda kushinda uchaguzi na hili ni muhimu sana, na ili kufanikiwa katika hayo yote, tunahitaji nidhamu na upendo katika kusimamia yale tunayotarajia.


“Tuwe tayari kwa chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, tusiache nafasi yoyote na tujiandae kwa nguvu zote kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani na lengo ni kushinda majimbo angalau 20 kati ya majimbo 31 katika kanda ya Nyasa,” amesema Sugu.


Kuhusu changamoto za kitaifa, Sugu amesema kwa sasa Taifa linakabiliwa na uhaba wa madaktari wakati mtaani kuna madaktari zaidi ya 3,000 wanaoendesha bodaboda wakati wananchi wanahitaji huduma yao.


“Taifa lina uhaba wa madaktari lakini tuna madaktari wasomi zaidi ya 3,000 wapo mtaani, wanaendesha bodaboda wakati wananchi wanahitaji huduma ya madaktari, wanakosa huduma hili hatuwezi kulikubali,” amesema Sugu.


Pamoja na mambo mengine, mwenyekiti huyo wa kanda, amesema kwa sasa chama kinarudi kwa wafanyabiashara ambao sasa wamekuwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha kuanzisha migomo.


“Chama chetu sasa kinarudi kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa na changamoto mbalimbali zinawafanya waanzishe hata migomo. Chadema inakwenda kujikita kwenye eneo hilo,” amesema Sugu.


Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Iringa, William Mungai amewasihi wajumbe wa baraza hilo kwenda kuunganisha nguvu ya vijana kutokana na nafasi kubwa waliyonayo ndani ya chama.


Amesema kwa sasa wana malengo makubwa ya kuwa na wagombea katika kata zote na vijiji vyote vya mkoa wa Iringa kwa asilimia 100.


“Tuna malengo makubwa na asilimia 100 ya kuwa na wagombea katika kata zote na vijiji vyote na hii sio kazi rahisi,” amesema Mungai.


Mapema akizungumza katika baraza hilo, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi amesema katika kipindi hiki wanahitaji kuwa wamoja kuliko wakati wowote, huku akiwasihi wajumbe hao kuhamasisha wananchi wajiandikishe kwenye daftari la Ä·udumu la wapigakura ili washiriki uchaguzi kwa kupiga kura.


Hata hivyo, chama hicho kimevuna wanachama wawili akiwemo mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Iringa, Abuu Changawa na aliyewahi kuwa mgombea wa ubunge kupitia chama NRA, Onesmo Chengerela ambao wamejitokeza na kujiunga na Chadema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad