Mwaka mpya wa fedha wa 2024/2025 umeanza kwa malalamiko ya wateja wa umeme kwa kuongezeka makato ya kodi ya majengo kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000, kwa maana ya ongezeko la Sh500 kwa mwezi wanaponunua umeme wa Luku.
Watumiaji wa umeme, hasa wale wanaonunua umeme kabla ya matumizi (Luku), wengi wenye matumizi madogo walijikuta kwenye taharuki kwa kushindwa kupata huduma hiyo kwa Sh2,000, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Kwenye makundi mbalimbali ya Tanesco yanayojumuisha wateja, tangu juzi kumekuwa na malalamiko hayo na wengine wakionyesha ujumbe kuwa fedha zao, kama Sh2,000 zimetumika kulipa kodi ya majengo, lakini umeme hawakupata.
Licha ya ufafanuzi uliotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwamba ongezeko hilo ni malipo ya deni walilopaswa kukatwa wateja Julai 2023, majibu hayo yalitakiwa kutangazwa kabla ya fedha kukatwa. Tunafahamu utendaji kazi mzuri wa kitengo cha mawasiliano cha Tanesco wa kutoa taarifa inapotokea dharura, lakini kwa makato hayo, shirika hilo halijawatendea haki wateja wake na lilipaswa kuwaomba radhi.
Kitendo kilichofanywa na Tanesco cha kukata Sh500 bila taarifa kwa kila mteja aliyenunua umeme, kilisababisha minong’ono mingi isiyokuwa na tija kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakiilaumu Serikali imeongeza kodi kimyakimya.
Pamoja na nia njema ya Tanesco, haikuwa na sababu ya kushindwa kutoa taarifa kupitia kitengo chao cha mawasiliano kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Tunasema ni vema Tanesco wakatoka hadharani kuomba radhi, sababu kuna watu waliozoea kutokana na kipato chao na matumizi madogo ya umeme, kununua umeme hata wa Sh500 na unawatosha kulingana na matumizi yao.
Umeme umekuwa msingi muhimu wa maendeleo katika maisha ya kila siku ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini na umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kuanzia nyumba za kawaida hadi viwanda vikubwa.
Ni wazi kwamba umeme unaboresha maisha ya kila siku ya wananchi kwa matumizi ya taa za nyumbani, kupikia chakula, kuhifadhi chakula kwenye friji, na hata kuendesha vifaa vya burudani kama televisheni na redio.
Wananchi wanaweza kupata habari na elimu kupitia intaneti, na hivyo kuboresha ufahamu wao na kuwa na fursa zaidi za kujifunza na kuboresha maisha yao, lakini pia wanafunzi wanaojisomea usiku kukosa mwanga kwa sababu ya ongezeko la kodi isiyokuwa na taarifa ni kuwanyima haki yao.
Kitendo kilichotokea hakipaswi kurejewa sababu baadhi ya watu walilazimika kulala gizani au kushindwa kufanya mambo mbalimbali ya dharura kwa kushindwa kununua umeme, kwani fedha hazikutosha.
Tunasema wateja wa Tanesco wanahitaji kupewa taarifa za dharura wakati wa matatizo, lakini hata pale kunapokuwa na jambo linalowahusu, lisifanyike bila kuwapa taarifa.
Wanachotakiwa kufahamu Tanesco ni kwamba kwa kutoa taarifa si tu kunawasaidia kufikisha ujumbe, lakini pia kunajenga uhusiano mzuri kati yao na wateja wao. Tanesco wanapaswa kufahamu kuwa wananchi wanajua shirika hilo ni tegemeo lao na wanapata faraja pale shirika linapowajali kwa kujibu mahitaji yao kwa haraka na ufanisi.
Hivyo basi, umuhimu wa Tanesco kuwajali wateja wake kwa kuwapatia huduma bora na kuwapa taarifa za dharura hauwezi kupuuzwa. Uhusiano mzuri kati ya shirika na wananchi unaimarisha ushirikiano na kujenga jamii imara na yenye ustawi.