SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limewatoa hofu wateja wake wa Dar es Salaam na Pwani kuhusu uboreshaji katika mfumo wa Luku kwamba kila mmoja atafi kiwa.
Kauli hiyo ya Tanesco imetokana na wasiwasi uliowakumba baadhi ya wateja wao walionunua umeme na hawakufanyiwa maboresho kama maelezo ya Shirika hilo yalivyosema.
Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Irene Gowele alisema tayari maboresho yameshaanza katika baadhi ya maeneo.
“Kwa upande wa Dar es Salaam tayari tumeshaanza tangu Julai 22 na tumewafikia wateja wa Kinondoni Kusini, Kaskazini na Ilala kidogo pengine mpaka wiki ijayo tutakuwa tumefikia wateja wengi zaidi,” alisema.
Alisema sababu ya kufanya maboresho hayo kwa awamu kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani ni wingi wao. “Tumejifunza kwenye mikoa tuliyopita, hivyo tumefanya marekebisho, unajua Dar es Salaam na Pwani inabeba wateja wetu karibu nusu na robo sasa hao wote tukisema maboresho yafanyike kwa pamoja haitawezekana kutokana na changamoto tulizopata mikoa mingine, lakini wote watafikiwa,” alisema.