Serikali ya Tanzania imekubali kuilipa kampuni ya Australia, Indiana Resources Limited fidia ya Dola milioni 90 za Marekani (sawa na Sh237 bilioni), baada ya kuafikiana kutokana na kampuni hiyo kunyang’anywa mradi wa Ntaka Hill Nickel wa madini ya sulfidi ya nikeli ulioko mkoani Lindi.
Awali, katika uamuzi uliotolewa Julai 14, 2023 na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) uliitaka Tanzania kuilipa Indiana Resources fidia ya Dola milioni 109 za Marekani (Sh260 bilioni), baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.
Serikali pia ilitakiwa kulipa fidia ya Dola milioni 76.7, sanjari na riba ya asilimia mbili iliyokokotolewa kuanzia Januari 10, 2018 baada ya kufunguliwa kesi hiyo, hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa Dola milioni 109.5 (sawa Sh260 bilioni kwa sasa).
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Indiana Resources Limited leo Jumatatu Julai 29, 2024 kiasi walichoafikiana kulipwa ndio hicho na hadi sasa, Tanzania imeshatoa malipo ya Dola milioni 35 (Sh94.5 bilioni).
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo na gazeti la The Citizen, alijibu kwa kifupi, “Ndio, ni kweli.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kampuni hiyo imekubali ofa kutoka Tanzania ambayo ni chini ya kiasi cha awali kilichotolewa na ICSID ambacho kilikuwa takriban Dola milioni 109 za Marekani, ili kuokoa muda na gharama za kufuatilia kesi za kubatilisha au usuluhishi na shughuli za utekelezaji.
“Tanzania itahitajika kukamilisha kiasi kilichobaki katika awamu mbili, Dola milioni 25 ifikapo Oktoba 25, 2024 na Dola milioni 30 ifikapo Machi 30, 2025.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro kati ya Indiana Resources na Tanzania ulitokana na mabadiliko ya Sheria za Madini za Tanzania mwaka 2017 na 2018.
Januari 10, 2018, kupitia kanuni zake za Haki za Madini za 2018, Tanzania ilitangaza kuwa leseni zote za uhifadhi zilizotolewa kabla ya tarehe ya kuchapishwa kwa kanuni hizo zilifutwa na zitakoma kuwa na athari za kisheria.
Leseni hizo zilikoma kuwa na athari yoyote ya kisheria. Haki za maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na leseni iliyokuwa kwa Indiana Resources zilihamishiwa kwa Serikali.
Hali hiyo iliathiri leseni ya uhifadhi ya Indiana Resources kwa mradi wa Ntaka Hill Nickel, uchunguzi na maendeleo ya madini ya sulfidi ya nikeli huko mkoani Lindi na kampuni hiyo ilikadiria thamani ya jumla ya hadi Dola milioni 217.
Leseni za uhifadhi ziliruhusu kampuni kumiliki baadhi ya maeneo yenye madini bila kuendeleza pale ambapo kulikuwa na vikwazo vya kiufundi, hali mbaya ya soko au sababu nyingine za kiuchumi.
Hata hivyo, Serikali ilieleza kuwa utaratibu huo ulikuwa wa kinyonyaji, kwani kampuni zingeshikilia maeneo makubwa bila kuyaendeleza au kuruhusu nchi kupata manufaa yoyote.
Kwa mujibu wa Indiana iliyokuwa ikimiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili za Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited, zilijaribu kuishawishi Serikali kurejesha leseni hiyo, lakini haikufanikiwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 ndipo ikawasilisha ombi la fidia ICSID.
Utekelezaji wa haraka wa kanuni hiyo uliigharimu nchi kwa kiasi kikubwa katika usuluhishi, kwani kampuni nyingi ikiwamo Indiana Resources zilidai kuwa zilipata hasara kubwa za kibiashara kutokana na uamuzi wa Tanzania ambao unalingana na kunyang’anywa kwa haki kinyume cha sheria.
Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano ya Mkataba wa Uwekezaji wa Tanzania (BITs) kati ya Tanzania na Uingereza chini ya uwekezaji wa kampuni hizo mbili za Uingereza.