Ufaulu Wapaa Kidato cha Sita, Walioingia na Simu Wafutiwa

 

Ufaulu Wapaa Kidato cha Sita, Walioingia na Simu Wafutiwa

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita na ualimu daraja A (GATCE) mwaka 2024, huku matokeo ya watahiniwa 24 yakifutwa kutokana na udanganyifu.


Matokeo hayo yametangazwa leo Jumamosi, Julai 13, 2024 na Katibu Mtendaji wa Necta katika ofisi za baraza hilo Zanzibar, Dk Said Mohamed amesema watahiniwa walibainika kuingia na simu kwenye vyumba vya mtihani, kukutwa na notisi na wengine kusaidiana kufanya mitihani.


Kati ya waliofutiwa matokeo hao 24, amesema watahiniwa 22 ni wa kidato cha sita, 17 wa shule na watano wa kujitegemea, mmoja wa mtihani wa ualimu daraja A na mmoja wa stashahda ya ualimu.


Kwa mujibu wa Dk Mohamed, tathmini ya udanganyifu inaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na imani yao itafika wakati itakwisha.


Katibu Mtendaji huyo wa Necta, amesema ufaulu wa jumla kwa masomo yote ni asilimia 96.84 huku somo lililoonekana kuendelea kuwa mwiba kwa watahiniwa ni Basic Alliance Mathematics (BAM) ambalo ufaulu wake ni asilimia 78.


Katika matokeo hayo, Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 326, kati ya hao 304 wa mtihani wa kidato cha sita, 12 wa ualimu na tisa mtihani wa stashahada ya ualimu wa sekondari wamezuiliwa kutokana na matatizo ya kiafya.


Hata hivyo, Dk Mohamed amesema vitendo vya udanganyifu katika mitihani hiyo vimeendelea kudhibitiwa na kupungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.


“Matukio ya udanganyifu wa kimkakati kwa sasa hayapo yameendelea kudhibitiwa na ndio maana unaona leo hata hatujatangaza shule yoyote ambayo imejihusisha na udanganyifu badala yake ni kutokana na wanafunzi wenyewe,” amesema Dk Mohamed.


Matokeo yalivyokuwa


Dk Mohamed amesema watahiniwa 113, 536 wa shule na kujitegemea walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Mei mwaka huu kati ya hao wasichana ni 50, 614 sawa na silimia 44.58 na wavulana 62,922 sawa na asilimia 55.42.


Kati ya watahiniwa hao watahiniwa wa shule walikuwa 104,454 na watahiniwa kujitegemea walikuwa 9,082.


Amesema kati ya watahiniwa 104, 454 wa shule waliosajiliwa watahiniwa 103,812 sawa na asilimia 99.39 walifanya mtihani, wasichana walikuwa 46,793 sawa na silimia 99.43 na wavulana ni 57, 019 sawa ana silimia 99.35. Watahiniwa 642 sawa na silimia 0.61 hawakufanya mtihani huo.


Ufaulu wa jumla


Kwa mujibu wa Dk Mohamed, watahiniwa wa shule waliofaulu ni 103,252 sawa na silimia 99.92 ya watahiniwa wenye matokeo, kati ya hao wasichana waliofaulu ni 46, 615 sawa na silimia 99.93 na wavulana ni 56,637 sawa ana silimia 99.91. watahiniwa walioshindwa mtihani ni 84 sawa na asilimia 0.08.


Mwaka 2023 watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa 96,319 sawa na asilimia 99.44 ya watahiniwa. hivyo waliofanya mtihani mwaka 2024 wameongezeka kwa asilimia 7.78.


Wasichana waongoza kwa ufinyu


Amesema watahiniwa 111,056 wa shule na kujitegemea sawa na asilimia 99.43 ya watahiniwa wenye matokeo ya mtihani wa kidato cha sita 2024, wamefaulu.


Wasichana waliofaulu ni 49,837 sawa na asilimia 99.61 wakati wavulana waliofaulu ni 61,219 sawa na asilimia 99.28. Mwaka 2023 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 104,549 sawa na asilimia 99.23. Hivyo, ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na mwaka 2023.


Ubora wa ufaulu


Ubora wa ufaulu kwa kuzingatia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha jumla ya watahiniwa 102,719 sawa na asilimia 99.40 wamepata ufaulu mzuri wa madaraja ya I-III.


Amesema watahiniwa wengi wapo katika ufaulu wa Daraja la I na II ambapo daraja la I ni watahiniwa 47,862 sawa na asilimia 46.32 na daraja la II ni 42,359 sawa na asilimia 40.99.


“Mwaka 2023 watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja I-III walikuwa 95,442 sawa na asilimia 99.30. Hivyo, ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.10 ikilinganishwa na mwaka 2023,” alisema


Watahiniwa waliopata ufaulu wa Daraja la I-II ni kati ya asilimia 94.20 hadi 95.95 katika tahasusi za lugha, Sayansi Jamii, Biashara na Uchumi na katika tahasusi za Sayansi Asilia watahiniwa waliofaulu Daraja la I-II ni asilimia 79.40.


Asilimia 66.69 ya watahiniwa wamepata ufaulu wa Daraja la III katika tahasusi za ualimu wa masomo ya sayansi na biashara.


Hata hivyo, idadi kubwa ya watahiniwa waliopata Daraja la I-II ipo katika tahasusi za Sayansi Asilia ikifuatiwa na tahasusi za Sayansi Jamii ambapo tahasusi za Sayansi Asilia ina watahiniwa 31,386 na tahasusi za Sayansi Jamii ina watahiniwa 30,126.


Kujikongoja somo la BAM


Takwimu za matokeo zinaonesha, masomo yote yana watahiniwa waliofaulu kati ya asilimia 96.84 hadi 100 isipokuwa somo la Basic Applied Mathematics ambalo watahiniwa wamefaulu kwa asilimia 77.55.


Hata hivyo, amesema ufaulu wa somo la Basic Applied Mathematics umeendelea kuimarika ambapo umeongezeka kwa asilimia 9.02 ikilinganishwa na mwaka 2023.


Idadi ya shule katika makundi ya Umahiri inaonesha kuwa, kati ya shule zote 929 zenye matokeo ya ACSEE 2024, shule 710 sawa na asilimia 76.43 zimepata wastani wa daraja la C ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu.


Shule zilizopata wastani wa daraja la A-C zimeongezeka kwa asilimia 6.25 kutoka idadi ya shule 709 sawa na asilimia 80.94 mwaka 2023 hadi kufikia idadi ya shule 810 sawa na asilimia 87.19 mwaka 2024.


Hata hivyo hakuna shule yenye wastani wa daraja la S au F.


Matokeo ya ualimu


Dk Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 7,944 sawa na asilimia 99.81 ya watahiniwa 7,959 wenye matokeo ya mtihani wa Ualimu Daraja la A mwaka 2024 wamefaulu.


Kati ya watahiniwa hao, Wanawake ni 4,384 sawa na asilimia 99.77 na Wanaume ni 3,560 sawa na asilimia 99.86.


Watahiniwa 4,494 sawa na asilimia 56.46 wamepata ufaulu wa daraja la tatu ‘Pass’ ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu.


Wadau


Wakizungumza kusuhu matokeo hayo baadhi ya wananchi walisema licha ya kuonyesha kuongezeka kwa ufaulu lakini upo kwenye nadharia kulio vitendo.


Abubakar Ismail mdau wa elimu alisema “Bado elimu yetu ipo kinadharia zaidi tunaambiwa leo ufaulu unapanda kila mwaka lakini mbeleni hatuoni hao wataalamu katika sekta nzito na za kibunifu kwa hiyo bado ipo haja serikali kuongeza mikakati ya kuboresha elimu yetu ili iwe kwa vitendo na shindani zaidi,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad