Taarifa ilizozipata Mwanaspoti zinabainisha kwamba, mpaka sasa Simba haijampa Chama barua ya kumuachia licha ya kwamba nyota huyo amemaliza mkataba wake ndani ya kikosi hicho.
Chama ambaye alianza kuitumikia Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya kwao Zambia, ameondoka Simba mwishoni mwa msimu uliopita baada ya mkataba wake kumalizika na kutambulishwa Yanga Julai Mosi, mwaka huu.
Mwanaspoti linafahamu kwamba, leo Jumanne, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inakutana pale kwenye ofisi za TFF zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam kupitia mashauri kadhaa yaliyopo mezani kwao.
Mtoa taarifa wetu amebainisha kwamba, miongoni mwa mambo ambayo leo yatajadiliwa, ni ishu ya Simba mpaka sasa kushindwa kutoa barua ya kumuachia Chama ili aidhinishwe rasmi ndani ya Yanga huku taarifa zikibainisha kwamba upande wa mchezaji ndiyo umewasilisha malalamiko hayo.
"Simba mpaka sasa hawajampa Chama barua ya kumuacha awe huru baada ya kumaliza mkataba nao, hili suala limefikishwa kwenye kamati na ni miongoni mwa yatakayojadiliwa katika kikao cha kesho (leo) pale TFF," kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti lilifanya juhudi za kuwasaka viongozi wa Simba na Yanga kuzungumzia ishu hiyo, lakini hawakuwa tayari kuweka wazi huku wakisubiri uamuzi wa kamati.
Mbali na ishu ya Chama, kamati hiyo pia itakutana leo kujadili sakata la beki Lameck Lawi ambaye Simba inasema ilimsajili kihalalaki wakati Coastal Union ikikomaa kwamba hakuna dili hilo.
Lawi anatajwa kusajiliwa Simba huku waajiri wake Coastal Union wakikiri kuwa bado ni mchezaji wao hivyo timu ambayo imemnunua mchezaji huyo imewasilisha malalamiko juu ya usajili wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Said Soud alisema ni kweli leo watakutana kujadili mashauri yote yaliyowasilishwa kwenye kamati yao.
"Kikao kitafanyika kesho (leo) lakini siwezi kuthibitisha ni kesi gani zipo mezani kwa sababu huwa tunakutana nazo siku ya tukio, kuhusiana na Lawi na mimi nimesikia kama ulivyosikia wewe," alisema na kuongeza;
"Kamati yetu ni sawa na wanasheria mahakamani kesi ambazo hawajawahi kuzisimamia wanakutana nazo maakamani tofauti na zile ambazo zimeshasikilizwa na kupangiwa tarehe nyingine."
Soud alisema wanakutana kujadili ikiwa ni utaratibu wao kukutana mara baada ya usajili kufanyika ili kupitia pingamizi zilizopo.
“Dosari kwenye suala la usajili huwa hazikosekani, sisi tunakutana kuangalia wapi kuna shida ili mambo yakae sawa,” alisema.
MSIKIE MAGORI
Licha ya Lawi kuendelea kusalia nchini wakati Simba ipo Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amekiri kuwa huyo ni mchezaji wao wanasubiri uamuzi wa kamati baada ya kupeleka malalamiko huko.
Alisema ni mchezaji wao kwani walifanya taratibu zote za malipo kwa ajili ya kumnunua lakini ghafla mambo yakaenda tofauti lakini hilo sasa lipo chini ya kamati husika, hivyo hawezi kulizungumzia sana.
"Msimamo wetu sisi Simba ni kwamba Lawi ni mchezaji wa Simba japo tunasubiri maamuzi ya kamati na kama yatatoka tofauti tutakata rufaa ili kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa haki." alisema Magori.