Hadi sasa sote tunajua, kuna juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha jamii inajitambua kiafya zao.
Mtu anapojitambua afya yake inamsaidia kujua jinsi ya kuishi, ikiwamo kujipanga katika suala zima la kimaisha, akitambua hatua hizo kiafya na namna ya kuisimama.
Pale anapojigundua ana hofu kutokana na kugundulika maambukizi ya virusi vya Ukimwi mapema, inakuwa msaada mkubwa.
Zamani katika hali ya kujificha na kutaka wasitambulike, wanajamii walisafiri kutoka sehemu moja, kwenda mkoa mwingine kuchunguzwa afya zao kama ana maambukizi hayo ya virusi vya Ukimwi au la.
Kadri muda ulivyopita na kuwapo uzoefu kuhusu changamoto hiyo, ikapatiwa aina fulani ya ufumbuzi, ambayo watu wanaenda katika vituo vya afya na kupima afya zao, kisha hata anapotambulika kuwa na shida hizo, hatua na uangalizi zaidi na matibabu yanafanyika.
Wakati fulani, ukaja utaratibu wa kuwapo vifaa vya kupima mwenyewe na hata mtu akiwa nyumbani anajipatia huduma hiyo. Ni tofauti na awali, ilikuwa lazima mtu afike katika kituo cha afya pekee, ndipo anapopatiwa vipimo hivyo.
Hayo yote kwa ujumla, ni maendeleo yanayoletwa na serikali, kupitia wadau kuhusiana na mustakabali wa kujali afya za Watanzania, kila mahali waliko, jumla yao wakiwa wastani wa milioni 612.7 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka juzi.
Hivi karibuni, umewekwa utaratibu mpya wa kitaifa wa upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa vipimo vitatu, ili kuthibitisha kuwa mtu kama mtu ana maambukizi ya VVU, hali inayosaidia kuongeza wigo na usahihi wa upimaji wake nchini.
Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi nchini, Dk. Ona Machangu, anasema ni sehemu ya magonjwa ya ngono. Akatamka katika kikao kinachohusu maradhi ya homa ya ini, pia akitambulisha mwongozo mpya kitaifa kuhusu upimaji virusi vya Ukimwi nchini.
Anasema, mtu atapimwa au kujipima na anapogundulika kuwa na virusi vya Ukimwi, katika kipimo cha awali, atalazimika kupata vipimo vingine viwili vya uhakiki, kuthibitisha ugunduzi wa awali, kabla ya hatua za matibabu kuanzishwa.
Dk. Machangu anasema lengo mahususi hapo la kutumia vipimo vitatu, ni kuhakikisha wigo wa upimaji unaongezeka kwa kupima vipimo ambavyo vitaleta majibu sahihi, zaidi yanayoleta manufaa na kusaidia huduma za uchunguzi kwa watu ili waweze kushawishika kupima na kuanza dozi mara moja endapo watagundulika.
Pia Dk. Machangu anasema, ili kufikia lengo la kutokomeza maambukizi mapya ya Ukimwi ifikapo mwaka 2030, Wizara ya Afya inalenga kuendelea kuboresha huduma za upimaji huo, ili kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma za upimaji na kujua hali yake ya kiafya.
"Tanzania tupo katika malengo ya kidunia ya 95 95 95 na kutokana na tafiti za viashiria zinaonyesha 95 ya kwanza ya upimaji. Kama nchi tupo asilimia 83 hivyo tunalengo hasa la kuhakikisha tunamfikia kila mtu na huduma za upimaji nchini," anasema.
Kauli ya mtaalamu huyo, inaenda mbali zaidi akitamka kwa kuusihi umma, kuendelea kujitokeza kupima afya zao, ili kutambua hali walizo nazo kiafya na kuanza dozi ya kupunguza makali ya VVU mara moja.
"Niwakaribishe Watanzania kufika kwenye vituo vya afya kupata huduma za upimaji pia kuna huduma za kujipima kwani ni vizuri kujua afya yako ili kufurahia maisha," anasema.
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Maria Kelly, anasema wao kama wadau wa maendeleo, wamejidhatiti kuendelea kusaidiana na serikali, kuhakikisha mpango huo wa upimaji unatekelezeka.