Waliofunika nyuso wavamia msiba, wapiga waombelezaji

 

Waliofunika nyuso wavamia msiba, wapiga waombelezaji

Wananchi wa Kitongoji cha Nsenya Kijiji cha Ilembo wilayani Mbozi mkoani Songwe wameingiwa na hofu, wakidai kuvamiwa na kujeruhiwa na kundi la watu bila kueleza sababu za kufanya hivyo.


Baada ya kupata taarifa za uvamizi huo jana Julai 11, 2024, mwandishi wetu amefika kijijini hapo kuzungumza na baadhi ya wananchi ambao wamekiri kuwepo kwa tukio lilitokea wiki iliyopita na kuwa hadi sasa sababu za uvamizi huo haujajulikana.


Leonard Fijabo ambaye ni miongoni mwa waliokutana na mkasa huo, amesema walivamiwa kwenye msiba wa Twaha Mwashibanda na kupigwa bila kujua sababu ya za kufanyiwa hivyo, jambo lililoleta taharuki kwa wananchi waliokuwa msibani.


Amesema, “nikiwa na wageni kwenye msiba nilipigwa kwa mateke, virungu, mikanda na fimbo hali ambayo wananchi tumekuwa na hofu na kuwa na mashaka na usalama wetu.


Akisimulia tukio hilo, Eunence Tuya amesema watu hao walifika kwenye kitongoji cha Nsenya na kwa namna walivyokuwa wamevaa haikuwa rahisi kutambuliwa kwani walijifunika nyuso zao.


Amesema hawakujua idadi wavamizi kwa kuwa ilikuwa usiku na wamefunika sura, hivyo wameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.


"Tumepigwa sana, tumefedheheshwa sana bila kujua sababu za uvamizi huo na kiongozi wetu wa kitongoji hakuwa na taarifa za msako wa kukamata wahalifu, tunaomba serikali itusaidie," amesema Amina.


Kaimu mwenyekiti wa Mtaa wa Kitovuni A Ilembo, Amani Kibona amesema uvamizi huo ulifanyika kwa saa moja kuanzia saa mbili usiku mpaka saa tatu.


Kibona amesema pamoja na kushambuliwa kwa kupigwa viboko wananchi wa kijiji hicho, wameibiwa bidhaa zao.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustini Senga amekiri kupokea taarifa za uvamizi huo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kubaini wahusika wa tukio hilo.


“Kuna kesi mbili za kushambuliwa zimefunguliwa. Tutahakikisha tunawasaka na kuwakamata wavamizi wote hata kama ni askari polisi, askari magereza au kundi la watu, watawafikishwa kwenye vyombo vya dola," amesema Kamanda Senga.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad