Yanga Yaifunga Kaizer Chiefs 4 Bila, Yatwaa Ubingwa wa Toyota Cup

 

Yanga Yaifunga Kaizer Chiefs 4 Bila, Yatwaa Ubingwa wa Toyota Cup


Yanga imemaliza kitemi ziara yake ya maandalizi huko Afrika Kusini baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs huku ikitwaa ubingwa wa mashindano maalum ya Toyota Cup.

Ushindi huo umekuja siku chache baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy kwenye mashindano ya Mpumalanga Cup ingawa ilianza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Augsburg.

Mabao yaliyoipa Yanga ubingwa, katika mchezo huo yamefungwa na Prince Dube dakika ya 24, Clement Mzize dakika ya 62 huku Stephane Aziz Ki akipachika mawili dakika ya 45 na 62.

Kichapo hicho kinakuwa cha kwanza kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi aliyekabidhiwa kikosi hicho hivi karibuni, baada ya kuachana na FAR Rabat ya Morocco aliyoachana nayo kufuatia kukosa ubingwa wa Ligi ya Morocco 'Botola Pro'.

Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji, aliachana na Yanga Juni 14, 2023, baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo kisha kuipeleka fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.

Kuondoka kwa Nabi viongozi wa timu hiyo wakamteua Muagentina, Miguel Gamondi aliyetambulishwa Juni 24, 2023 huku msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake, akakipa kikosi hicho ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la FA.

Baada ya michezo hiyo ya Afrika Kusini, Yanga inarejea hapa nchini kujiandaa na tamasha la kilele cha wiki ya Mwananchi ambacho kinatarajiwa kuhitimishwa rasmi Agosti 4, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo la Wiki ya Mwananchi litakapohitimishwa ndipo macho na masikio yataelekezwa katika mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya timu hiyo dhidi ya Simba utakaopigwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo, ikiwa Afrika Kusini Yanga ilianza kushiriki michuano ya Mpumalanga Premier international Cup 2024 ambapo ilianza kwa kichapo cha mabao 2-1, dhidi ya Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu 'Bundesliga'.

Baada ya kichapo hicho, Yanga ikasawazisha makosa hayo kwani mchezo uliofuatia dhidi ya wenyeji, TS Galaxy ya Afrika Kusini ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota mpya wa timu hiyo, Prince Dube aliyejiunga nayo msimu huu akitokea Azam FC.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad