Askari Watano Wadaiwa Kumbaka Binti, Walitumwa na Bosi





Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishani Msaidizi David Misime.
BINTI ambaye umri wake haujatajwa, mkazi wa Mtaa wa Msakala na Dovya, jirani na Shule ya Msingi Yombo Dovya, wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam, anadaiwa kubakwa na kulawitiwa na vijana watano ambao wanadaiwa ni askari wa moja ya vikosi vya ulinzi nchini.

Vijana hao walimpiga picha mjongeo wakati wanamfanyia ukatili huo binti huyo kisha kuisambaza katika mitandao ya kijamii, wakidaiwa kutumwa na bosi wao aliyedai kuwa binti huyo ana uhusiano wa kimapenzi na mumewe.

Tukio hilo liliibuliwa na aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye aliandika mkasa mzima kwenye ukurasa wake wa X huku akiwatumia nakala (tag) Rais Samia Suluhu Hassan kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Tanzania, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Stergomena Tax na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima.

Meya Boniface aliandika: "Binti huyu amebakwa na kulawitiwa akiwa anarekodiwa video tatu tofauti. Askari hao walimrekodi wakiwa wanambaka na kumlawiti, wamesambaza video zake mitandaoni kwa maagizo ya kiongozi wao (afande) ambaye amewatuma kumpatia huyu binti adhabu.

“Kwa maelezo ya vijana hao (askari), kosa la huyu binti ni kutembea na mume wa bosi wao (afande), Mahojiano katika video hizo tatu tofauti yanaonesha binti amekamatwa na kubakwa na kulawitiwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam," alidai Jacob.

Anadai kuwa afande huyo aligundua kuwa mume wake ana uhusiano na binti huyo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi waliokuwa wanawasiliana, ndipo alichukua simu ya mume wake na kuendelea kuwasiliana na binti kwa ujumbe wa kimapenzi.

Meya huyo wa zamani anadai kuwa mwanamke huyo aliwasiliana na binti huyo na kukubaliana kukutana na kumtumia fedha za nauli ndipo binti alichukua usafiri kwenda alikoelekezwa na alipofika, aliwasiliana na mwenyeji wake ambaye alimwelekeza aliko na alipofika, alipokewa na vijana hao kisha kupelekwa eneo walikomtenda ukatili huo.

Meya huyo mstaafu anaendelea kudai kuwa: "Sisi Watanzania tuliohuzunishwa na ukatili huu, tunataka kuona vijana wote watano na kiongozi aliyewatuma wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.


"Kuona majeshi yetu yenye heshima kubwa sana barani Afrika, yanajitenga na kashfa hii ya ubakaji kwa raia wake. Majeshi na vikosi vyote vinafanya msako na utambuzi wa watu hawa, kisha wawakabidhi katika vyombo vya kisheria na kushtakiwa kama kweli ni waajiriwa wa majeshi yetu.

"Kwa kuwa Amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ni mama, Waziri wa Ulinzi ni mama, Waziri wa Wanawake ni mama, tunatarajia kuona wakichukizwa zaidi juu ya udhalilishaji na ukatili juu ya mtoto wa kike wao wakiwa kama wazazi na viongozi wenye dhamana ya kulinda raia wa Tanzania," Jacob anasema.

JESHI LA POLISI

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishani Msaidizi David Misime, jeshi hilo linafanyia kazi taarifa za tukio hilo.


"Kwenye mitandao ya kijamii inaonekana video inayosambazwa ikimwonesha binti anayesemekana ametokea Yombo Dovya, Jiji la Dar es Salaam akidhalilishwa na kufanyiwa ukatili ambao haukubaliki kwani ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na haki za binadamu," Kamishna huyo alisema katika taarifa yake hiyo.

Kamishna Msaidizi Misime alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kuendelea kusambaza video hiyo kwa kuwa kusambaza ni kosa kisheria, pia ni kuendelea kudhalilisha utu wa binadamu.

"Pia tunatoa wito kwa mwenye taarifa ya kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia kwa haraka waliofanya ukatili huu, asisite kutusaidia kwa kutupa taarifa au kumpatia kiongozi yeyote yule wanayemwamini kwamba taarifa ikimfikia watu hao watapatikana haraka iwezekanavyo au toa taarifa kupitia namba 0699998899," alisema.

WAZIRI GWAJIMA

Katika ujumbe huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima aliandika jana: "Ahsante sana kunaTag. Nimesoma na kuwasilisha kwenye mamlaka yenye dhamana ya kuchunguza na kukamata ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Watatoa taarifa kwa nafasi yao.

"Kwa namna yoyote ile, taarifa hii inasikitisha na jambo kama hili halifai, ni la kulaaniwa na haliwezi kufumbiwa macho. Iwapo manusura au aliyekaribu naye atasoma hizi taarifa, wasiogope, watoe taarifa ili manusura apate msaada haraka, ikiwamo huduma za afya, kisaikolojia na usalama.

"Namba zetu ziko hewani, yangu mwenyewe ni… (akataja namba zake za simu) na za wizara ziko kwenye tangazo letu.

"Aidha, tuvipe ushirikiano vyombo vyetu kila mwenye taarifa namba za IGP alizotangaza ni… (akataja namba za simu). Asanteni, tuendelee kushirikiana kulinda jamii yetu. Sisi ni jamii moja, uovu hapana!"

Waziri Dorothy pia alisema akiambatanisha taarifa ya Jeshi la Polisi kwenye ukurasa wake na kuandika: "Kwa kurejea taarifa ya Jeshi la Polisi, ndugu wanajamii, tuendelee kutoa ushirikiano sasa na daima. Asanteni sana, Asanteni sana."

Baada ya ujumbe huo, wananchi waliendelea kuandika ujumbe, wakimpongeza kwa kuwa na utaratibu wa kufanyia kazi haraka taarifa anazopewa.

"Wewe mama (Gwajima) ni mtu makini sana kati ya mawaziri tulionao. Hili jambo si la kuachiwa raia tupige kelele wenyewe. Kila mpendahaki anapaswa kupaza sauti. Mungu akuongezee maarifa na hekima," aliandika mmoja wa waliosoma ujumbe wa waziri huyo.

WANAHARAKATI

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema wanalaani tukio hilo huku wakieleza kuongezeka matukio ya vyombo vya ulinzi kujichukulia sheria mkononi panapotokea tofauti baina yao na raia.

Alisema ni muhimu kukawa na mwongozo kwamba waache kutumia vibaya madaraka yao kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria na inapotokea wamekosana na raia, zifuatwe taratibu na si kutumia nguvu na kuumiza raia, jambo linalosababisha utawala wa sheria kutoheshimiwa.

"Tunapokea malalamiko mengi ya kundi hili kuwatendea ubaya raia, kukiwa na mgogoro wa ardhi, hivi karibuni kuna tukio la askari huko Mkuranga alihisi raia anatembea na mkewe, alikusanya wenzake wakakamata raia wakawapiga, lakini kuna tukio la mwanajeshi kumpiga dereva wa daladala.

"Ni muhimu viongozi wakakemea vikali haya matukio haya kuondoa dhana kwamba mtu akiwa mwanajeshi/askari anaweza kufanya jambo lolote kwamba wako juu ya sheria. Tunataka wahusika wa tukio hili wakamatwe na wafikishwe kwenye mahakama kwa uwazi na si usiri," alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Ananilea Nkya, alisema waliotenda tukio hilo wamekiuka Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998, hivyo lazima polisi wawakamate kisha wapelekwe mahakamani ili haki ipatikane.

"Hakuna mtu aliye juu ya sheria, hakuna sababu yoyote kwa Jeshi la Polisi kuogopa kumkamata yeyote aliyetenda ukatili huo, kila mmoja ana wajibu wake na hivyo lazima sheria ziheshimiwe na hatua kali zichukuliwe mara moja na kuwafikisha mahakamani.

"Hakuna sababu yoyote inayohalalisha mtu kubakwa. Kubaka mtu ni kosa la jinai, jinai ikitendeka lazima hatua zichukuliwe. Hatua zisipochukuliwa itaonyesha kuna watu wako juu ya sheria, jambo ambalo ni hatari sana kwa nchi yetu," alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia tukio hilo, alisema:

"Inasikitisha kuwa wanaotakiwa kulinda haki ndiyo wanavunja haki. Jambo hili si tu ni jinai, bali pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

"Kama mume amechepuka, kuna Sheria ya Ndoa (1971), hivyo angeomba talaka au kumsamehe, na si kumfanyia ukatili. Habari hii ikithibitika, wote wachukuliwe hatua za kisheria maana hakuna aliye juu ya sheria. Tutaifuatilia kesho (leo) ili tumpe huyu binti msaada wa kisheria."

Source: IPP Media

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad