Baba mzazi wa Aliyechoma PICHA ya Rais Amtaka Mwanawe akiwa hai au mfu

 

Baba mzazi wa Aliyechoma PICHA ya Rais Amtaka Mwanawe akiwa hai au mfu

Mkazi wa Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Yusuph Chaula (56) amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la mwanawe Shadrack Chaula kutekwa na watu wasiojulikana.


Shadrack anadaiwa kutekwa na watu hao Agosti 2, 2024 ikiwa ni takribani siku 20 kupita tangu alipotoka Gereza la Ruanda Mkoa lililoko mkoani Mbeya, alipokuwa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya Sh5 milioni.


Kijana huyo mwenye miaka 24 alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya na kuhukumiwa kifungo hicho baada ya kukiri kosa la kuchoma picha ya Rais.


Baada ya kukiri kosa hilo, Julai 4, 2024 Mahakama hiyo ilimtia hatiani Shadrack kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.


Agosti 2, 2024 katika mitandao ya kijamii kulikuwa na taarifa zinazoeleza katekwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari nyeusi kisha kuondoka naye na jitihada za kumtafuta zilikuwa zikiendelea kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga


Leo Jumatano, Agosti 7, 2024, baba mzazi wa Shadrack amezungumza na Mwananchi iliyotaka kujua nini kinaendelea au kama kuna taarifa zozote amezipata juu ya mwanawe.


Katika mazungumzo yake, Chaula amelezea tukio la kijana wake akisema ilikuwa saa 2 asubuhi ya Agost 2, 2024 akiwa kwenye eneo lake la biashara alibebwa kindakindaki (kibabe) na watu wasiojulikana kwa kuingizwa kwenye gari nyeusi kisha ilielekea maeneo ya jijini Mbeya.


"Naomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mwanangu apatikane akiwa hai au amekufa maana kutekwa ni sawa na tukio la kuchinjwa kwa mtu," amesema.


Amesema baada ya kupata taarifa za kukekwa kwa mwanawe amefanya jitihada mbalimbali kumtafuta kwa ndugu na jamii, hosptalini ambazo hazijazaa matunda na kulazimika kuomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kufanikisha apatikane akiwa hai au mfu.


Amesema kadri siku zinavyokwenda anapata shaka kwa kuwa mazingira ya kuchukuliwa mwanawe siyo ya kistaarabu kutokana na kuchukuliwa kindakindaki.


"Awali, mwanangu Shadrack nikiri alifanya ukorofi baada ya kutenda kosa la kuchoma picha ya kiongozi mkuu wa nchi, sheria zilitenda haki alihukumiwa miaka miwili katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe," amesema.


Amesema katika hukumu huyo Mahakama ilimtaka kulipa faini ya Sh5 milioni, Watanzania wenye mapenzi mema walimchangia na kumtoa gerezani baada ya kukaa siku kadhaa.


"Nakumbuka kauli ya mwanangu baada ya kutoka gerezani alisema baba nawashukuru Watanzania kwa kunitoa kwenye kutumikia kifungo cha miaka miwili, sisi tungepata wapi kiasi hicho cha fedha," amesema.


Baba huyo amesema mwanawe mbali na kuwa msanii wa uchoraji, alikuwa akijihusisha na biashara ya duka na kuwa na maeneo mawili ya kuoshea magari katika Kijiji cha Ntokela huku akishilikiana vyema na vijana wenzake.


"Alikuwa ni kijana mtiifu sana na hata kuishi vizuri na wenzake na ndio maana alipobebwa na watu wasiojukana walikimbia kuleta taarifa, pia hata lile tukio lililosababisha kuhukumiwa tulishtushwa," amesema.


Amesema kwa sasa yuko njia panda aelewi wapi aende kufuatilia na kuomba Serikali kumsaidia apatikane akiwa hai au mfu.


Wakati baba akieleza hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Agosti 7, 2024 amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kubaini uhalisia.


"Tunaendelea na uchunguzi wa kina kubaini uhalisia wa tukio hilo, ingawa baada ya kuhukumiwa kuna watu walijichangisha fedha na kumtoa gerezani na kwenda naye jijini Dar es Salaam na suala la kurejea kijijini hapo linaleta utata," amesema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad