BAVICHA wajitosa sakata la ‘kutekwa’ aliyechoma picha ya Rais

 

BAVICHA wajitosa sakata la ‘kutekwa’ aliyechoma picha ya Rais

Wakati giza likiendelea kutanda kuhusu alipo Shadrack Chaula anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema litatumia siku ya vijana dunia kutangaza hatua watakazozichukua ili kukomesha vitendo hivyo.


Bila kuzitaja hatua hizo, mratibu wa uhamasishaji wa Bavicha, Twaha Mwaipaya ameiambia Mwananchi leo Alhamisi Agosti 8, 2024 kuwa uamuzi watakaoutangaza Agosti 12 (siku ya vijana dunia) huenda ukawa mwarobaini wa kukabiliana na vitendo vya utekaji vilivyoanza kurejea katika siku za hivi karibuni.


“Hatima ya Chaula na wengine waliotekwa akiwemo Kombo Mbwana (Tanga) itajulikana Agosti 12, haijalishi Shadrack atakuwa yupo huru au amekufa.


“Vijana wasiopungua 10,000 nchi nzima tutakutana Uwanja wa Ruanda Nzovwe Mbeya ili kukomesha vitendo hivi, tutaelezana namna kuvuka mto baada ya kufika mtoni,” amesema Mwaipaya.


Chaula (24) anadaiwa kutekwa na watu hao Agosti 2, 2024 ikiwa ni takribani siku 20 kupita tangu alipotoka Gereza la Ruanda mkoani Mbeya, alipokuwa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya Sh5 milioni.


Inadaiwa siku hiyo, katika mitandao ya kijamii kulikuwa na taarifa zilizoeleza Chaula alitekwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari nyeusi kisha kuondoka naye.


Kijana huyo mwenye miaka 24 alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe mkoani humo na kuhukumiwa kifungo hicho, baada ya kukiri kosa la kuchoma picha ya Rais.


Baada ya kukiri kosa hilo, Julai 4, 2024 Mahakama hiyo ilimtia hatiani Shadrack kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.


Mwaipaya ambaye alikuwa miongoni mwa wanaharakati waliofanikisha michango ya kumwezesha Chaula kulipa faini ya Sh5 milioni ili kuachiwa huru, amesema kijana huyo amefikisha siku ya sita bado hajulikani alipo.


“Tumewasiliana na baba yake (Yusuph Chaula) na ndugu zake muda wote wanalia kwa sababu hawajui kijana wao yupo wapi, bora mwanzo walijua mtoto wao yupo gerezani, ila sasa hawajui yupo katika kituo cha polisi, amekufa au kutupwa msituni.


“Maumivu walionayo wazazi wa Chaula ni makubwa kuliko alivyokuwa awali (gerezani). Awali wazazi walijua Chaula atamaliza kifungo atarejea lakini sasa hivi hajui mtoto wao yupo wapi,” amesema Mwaipaya.


Jana Jumatano Agosti 7, 2024 baba wa kijana huyo, Yusuph Chaula alizungumza na Mwananchi juu ya kutoonekana kwa kijana wake na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la mwanawe anayedaiwa kutekwa.


“Naomba Serikali ya Rais Samia kuingilia kati mwanangu apatikane akiwa hai au amekufa maana kutekwa ni sawa na tukio la kuchinjwa kwa mtu,” amesema Yusuph.


Mwaipaya amesema Agosti 12 kuna maadhimisho ya siku ya vijana yatakayofanyika mkoani Mbeya yakikutanisha wadau mbalimbali kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Kwa mujibu wa Mwaipaya, katika maadhimisho hayo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe atashiriki na wanaharakati wa haki za binadamu akiwemo Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi.


Wakati yakiendelea jana Jumatano, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alipoulizwa na Mwananchi kinachoendelea, alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kubaini uhalisia.


“Tunaendelea na uchunguzi wa kina kubaini uhalisia wa tukio hilo, ingawa baada ya kuhukumiwa kuna watu walijichangisha fedha na kumtoa gerezani na kwenda naye jijini Dar es Salaam na suala la kurejea kijijini hapo linaleta utata,” amesema Kamanda Kuzaga.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad