Bilionea wa Afrika Kusini Ampiku Dangote kama mtu Tajiri zaidi barani Afrika

 

Bilionea wa Afrika Kusini Ampiku Dangote kama mtu Tajiri zaidi barani Afrika

Bilionea wa Afrika Kusini, Johann Rupert amempiku mfanyabiashara wa viwanda kutoka Nigeria Aliko Dangote kama mtu tajiri zaidi barani Afrika, kulingana na data ya hivi karibuni kutoka kwa Bloomberg Billionaires Index.


Bw Rupert anadhibiti Richemont, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya bidhaa za anasa duniani, ambayo inamiliki chapa kama vile Cartier na Montblanc.


Thamani yake imepanda kwa $1.9bn hadi $14.3bn, na kumfanya kuwa katika nafasi ya 147 duniani, nafasi 12 mbele ya Bw Dangote.


Utajiri wa bwana Dangote umepungua kwa $1.7bn (£1.3bn) mwaka huu, na kufikia $13.4bn, Bloomberg inaripoti.


Kushuka kwa utajiri wa Bw Dangote kunadhihirisha mazingira magumu ya kiuchumi ya Nigeria, ambapo kampuni zake zinaendesha shughuli zake.


Tangu Rais Bola Tinubu ashike madaraka mwaka jana, ameanzisha mabadiliko kadhaa ya kiuchumi katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, ambayo imechangia mfumuko mkubwa wa bei, ambao kwa sasa ni zaidi ya 30%.


Bw Tinubu alisema mabadiliko hayo ni muhimu ili kupunguza matumizi ya serikali na kuchochea ukuaji wa muda mrefu.


Kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya naira kumemuathiri pakubwa Bw Dangote, ambaye utajiri wake unahusishwa kwa kiasi kikubwa na mali zinazotumiwa katika sarafu ya nchi hiyo.


Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijipatia utajiri wake katika viwanda vya saruji na sukari - na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha kiuchumi cha Nigeria, Lagos.


Himaya yake ya biashara, Kundi la Dangote, pia limekabiliwa na matatizo mengi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kucheleweshwa kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa . Aliorodheshwa na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi nchini humo.


Lakini ripoti ya hivi punde ya Bloomberg inamweka nafasi ya pili barani Afrika na ya 159 duniani.


'Sina nyumba nje ya Nigeria' - Dangote Dangote aliwashangaza wengi nchini Nigeria baada ya kusema hana nyumba nje ya nchi hiyo.


Bw Dangote alisema alikuwa na nyumba mbili - katika mji aliozaliwa wa Kano, na Lagos - na aliishi katika nyumba ya kukodi kila anapotembelea mji mkuu, Abuja.


Maoni yake yaliwashangaza wengi katika nchi ambayo watu matajiri wana sifa ya maisha yao ya kifahari.


Wanigeria wengi matajiri wanamiliki nyumba London, Dubai na Atlanta.


Matamshi yake yalizua hisia nyingi kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakisema ni uamuzi wa busara wa kibiashara kwani ni nafuu kulipa karo kuliko kununua nyumba.


Kwa Bw Dangote, sababu kuu ni kwamba amekuwa akitaka Nigeria kukua kiuchumi.


"Sababu ya kutokuwa na nyumba ya London au Marekani ni kwa sababu nilitaka kuangazia ukuaji wa viwanda nchini Nigeria," alisema.


Kupanda kwa thamani ya Bw Rupert kulichangiwa na utendaji mzuri katika sekta ya bidhaa za anasa.


Mbali na kampuni ya Richemont yenye makao yake Uswizi, hisa zake nyingine ni pamoja na Remgro, gari la uwekezaji la Afrika Kusini lenye hisa katika makampuni zaidi ya 30, Bloomberg inaripoti.


Nicky Oppenheimer, bilionea mwingine wa Afrika Kusini, aliorodheshwa kuwa mtu wa tatu tajiri zaidi barani Afrika akiwa na utajiri wa $11.3bn, akifuatiwa na Nassef Sawiris, mfanyabiashara wa Misri, mwenye utajiri wa $9.48bn.


Mwekezaji wa Afrika Kusini Natie Kirsh alikamilisha orodha ya mabilionea watano bora wa Afrika na $9.22 bn.


Kama Forbes, orodha ya matajiri ya Bloomberg hufuatilia mabadiliko ya kila siku katika thamani halisi ya watu matajiri zaidi duniani.


Taji la mtu tajiri barani Afrika linaweza kuendelea kubadilika huku hali ya soko ikibadilika wakati biashara zikikabili changamoto tata.


Je, Johann Rupert ni nani? Johann Rupert ni mwenyekiti wa kampuni ya bidhaa za kifahari ya Uswizi Compagnie Financiere Richemont kwa mujibu wa Forbes.


Kampuni hiyo inajulikana zaidi kwa chapa za Cartier na Montblanc.


Ilianzishwa mwaka wa 1998 kupitia msururu wa mali inayomilikiwa na Rembrandt Group Limited (kwa sasa ikiitawa Remgro Limited), ambayo babake Anton aliunda katika miaka ya 1940.


Anamiliki 7% ya kampuni ya uwekezaji mseto ya Remgro, ambayo ni mwenyekiti, pamoja na 27% ya Reinet, kampuni inayomiliki uwekezaji iliyoko Luxembourg.


Rupert amekuwa mpinzani mkubwa wa mipango ya kuruhusu fracking katika Karoo, eneo la Afrika Kusini ambako anamiliki ardhi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad