Bao moja la Clatous Chama katika ushindi wa mabao 4-0 ambao Yanga iliupata dhidi ya Vital'O ya Burundi, Jumamosi Agosti 17, 2024 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, limemfanya nyota huyo kutoka Zambia kuandika rekodi mbili huku akiboresha nyingine ya tatu.
Chama alifunga bao hilo katika dakika ya 68 akiunganisha mpira uliogonga mwamba na kurudi uwanjani ambao ulitokana na shuti lililoupigwa na Stephane Aziz Ki.
Kwa kufunga bao hilo, Chama sasa amefikisha mabao 22 kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na anazidi kutamba kwenye 10 bora ya wafungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo.
Rekodi ya kwanza Chama ambayo ameiweka ni ya kuwa mchezaji pekee aliyewahi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali alikuwa sawa na Mbwana Samatta aliyefumania nyavu mara 21 lakini kufunga bao hilo moja juzi kumemfanya aandike rekodi mpya.
Chama pia ameandika rekodi yake mwenyewe ya kuwa mchezaji anayeshika nafasi ya saba kwa kufunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka ile ya nane aliyokuwepo awali.
Anayeongoza chati ya ufungaji bora wa muda wote kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni nyota wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya DR Congo, Tresor Mputu ambaye amefunga mabao 39.