Kocha Mkuu wa Azam SC, Youssouph Dabo amesema kuwa licha ya kushindwa kupata matokeo mbele ya JKT Tanzania, jambo hilo halimpi presha ya kufukuzwa na mabosi wa klabu hiyo kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti.
Dabo amesema hayo baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyopigwa katika Dimba la Meja Jenerali Isamhuyo ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana huku akiwa na kumbukumbu ya kutolewa kwenye michuano ya CAFCL katika hatua ya awali na APR wiki iliyopita.
“Kabla sijaja Azam nilikuwa kocha na baada ya kuondoka Azam nitaendelea kuwa kocha, sina presha kuhusu kinachoendelea kama ambavyo jana nimeona waandishi wanazungumza. Mimi ni mtu ambaye ninafanya kazi kuendana na presha kwa sababu soka ni kitu ambacho kipo rohoni mwangu.
“Nitamalizana na Azam baada ya kumalizika kwa msimu huu labda nitaondoka ama nitaendelea kusalia na Azam lakini sina presha. Hii ni mechi ya kwanza lazima tutafute majibu ya changamoto zetu ili tuweze kufanya vizuri kwenye michezo ijayo,” amesema Dabo.