Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said amesema kuwa malengo ya klabu hiyo msimu huu kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ni kufika hatua ya robo fainali lakini endapo watakwenda mbele zaidi ya hapo basi itakuwa kama bonus.
Hersi amesema kuwa kwa namna anavyokiona kikosi chake bado hawezi kukipa nafasi ya kuchukua ubingwa huo kwani bado anakitengeneza mpaka kifike level kubwa ya kuchukua taji hilo kubwa barani Afrika.
“Changamoto kubwa ambayo tuko nayo ni kuimarisha kikosi ambacho kinaweza kukupa matokeo kwenye hali zote. Msimu uliopita wakati tunakwenda kwenye robo fainali ya CAFCL tuliwakosa wachezaji watatu muhimu dhidi ya Mamelodi Sundowns, hawa ni Yao, Pacome na Aucho, kwa hiyo kukosa upana wa kikosi kwenye hatua hiyo utaishia kupoteza mchezo. Tumejifunza tukasema msimu huu tuongeze wachezaji bora na wenye uzoefu ili tupate nafasi ya kusonga mbele.
“Sisi malengo yetu msimu huu ni kufika robo fainali, tunataka tuingie makundi kwanza tuzoee makundi, tukitoka hapo tuingie robo fainali na ndiyo malengo yetu. Lakini Mwenyezi Mungu huwa ana zawadi, akitupa zawadi ya kufika fainali au kuchukua ubingwa tutashukuru.
“Kikosi hiki cha Yanga bado hakijakamilika, kwenye dirisha hili kubwa kulikuwa na mchezaji ambaye tulitakiwa kumleta, kwa bahati mbaya hiyo dili haikukamilika, na baada ya hapo Januari (dirisha dogo) kutakuwa na ongezeko la wachezaji wengine wawili wa kimataifa. Kwa hiyo Yanga bado haijakamilika, siku ikikamilika ndiyo utatuuliza kuhusu fainali ubingwa wa CAFCL, lakini kwa sasa bado,” amesema Eng Hersi Said.