Mshambuliaji wa Simba, Fredy Michael ametabiriwa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku Kibu Denis akisamehewa na wana Msimbazi baada ya sakata lake la kutojiunga na kambi ya kikosi hicho iliyofanyika Misri.
Awali, Kibu alipewa likizo ya muda na uongozi akaenda Marekani kwa mapumziko kabla ya kurejea nchini na kisha kutimkia Norway kwenda kuzungumza na timu moja ya huko ili imsajili bila idhini ya waajiri wake.
Akizungumza juzi katika kilele cha tamasha la 'Simba Day', Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally kwenye utambulisho wa wachezaji watakaokitumikia kikosi hicho msimu ujao, amesema hakuna upinzani kwamba Fredy atachukua kiatu cha ufungaji bora.
"Haina ubishi bila shida yoyote huyu ndio mfungaji bora msimu huu, atafunga sana Msimbazi," Amesema Ahmed.
Wakati anatabiri hayo kwenye utambulisho, amesema Kibu wana Simba wamemsamehe kwa kile walichokiita utovu wa nidhamu baada ya kutojiunga na kambi.
"Sisi kama mashabiki tumekusamehe... ndugu wakigombana shika jembe ukalime, tumemaliza ugomvi na msimu huu bado yupo sana," amesema Ahmed.