Gamondi Ataka Rekodi Mpya Ligi Kuu Msimu huu

 

Gamondi ataka rekodi mpya Ligi Kuu msimu huu

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema moja ya falsafa anazokuja nazo msimu ujao ni kutoruhusu bao kirahisi kwenye mchezo wowote ambao timu yake itacheza.


Akizungumza jijini Dar es Salaam, alisema timu yoyote inayotaka kushinda mchezo wa mpira wa miguu ni lazima kwanza ihakikishe ina safu bora ya ulinzi ili kutoruhusu mabao rahisi na ya kizembe, hivyo msimu huu pamoja na ubora wa kikosi chake, lakini atahakikisha hilo halitokei.


Alisema hata kama litatokea, basi iwe ni nadra na sababu inayojitosheleza na si uzembe wa timu au mchezaji mmoja mmoja.


"Moja kati ya vitu ambavyo makocha wengi hawapendi ni kuona timu yake inaruhusu mabao kirahisi na kizembe, na tunakwenda kucheza mechi ngumu za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika, huko michezo ni migumu na watu wanatumia sana makosa madogo madogo kukuadhibu, hivyo tunaanza kulifanyia kazi kwenye Ligi Kuu," alisema.


Hata hivyo, alisema pamoja na hayo yote, lakini hatobadilika kwenye falsafa yake ya kuuchezea mpira na kushambulia, badala yake atawataka wachezaji wake kuwa makini na kushirikiana wanapokuwa wanazuia na wala isitafsiriwe kama atakuwa nyuma ya mpira.


"Bado nitacheza vile vile, sitobadilika kiuchezaji, watu wataiona Yanga ile ile ya msimu uliopita na inawezekana ikawa imara zaidi, sisi tunacheza mpira ambao kila mchezaji anashambulia, kila mmoja anakimbia, kila mmoja anajaribu kurudi haraka kukaba tunapopoteza mipira," alisema Gamondi raia wa Argentina.


Wakati kocha huyo akisema hayo, Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, amewataka wanachama na mashabiki kujitokeza kwa wingi msimu huu kwenye viwanja mbalimbali ili kuiunga mkono timu yao.


Meneja huyo alisema kama ambavyo mashabiki wamefanya msimu uliopita na kujichukulia tuzo ya kuingiza mashabiki wengi uwanjani, amewataka kuvunja rekodi ya mashabiki msimu unaoanza Ijumaa wiki hii.


"Timu iko vizuri sana, na inawezekana kuliko hata msimu uliopita, sasa hivi kikosi ni kipana zaidi, yaani kocha anaamua tu nani acheze, hana presha, kwa hiyo mashabiki nao wasiwe na presha, wajitokeze kwa wingi iwe hapa Dar es Salaam au mikoani," alisema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad